Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, October 6, 2011























































HATIMAYE the super business icon ndani ya muziki wa Bongo Fleva, Abdul Naseeb ‘Diamond’ (pichani chini) ametegua kitendawili cha ‘sapraizi’ yake kwa mpenzi wake Wema Isaac Sepetu kwa kumvisha pete ya uchumba, Risasi Mchanganyiko lina mkoba wenye mafaili yenye kila kitu.

 Ishu nzima iliyoshuhudiwa na paparazi wetu ilichukua nafasi wikiendi iliyopita, ndani ya ukumbi wa kijanja Bongo, Club Maisha uliopo pande za Masaki, jijini Dar es Salaam katika shoo ya kihistoria iliyopewa jina la ‘Happy Birthday Diamond’.


Shoo hiyo iliyokuwa na mashabiki kibao, kila mtu alionekana kutaka kujua Diamond atamfanyia nini mpenzi wake huyo baada ya vyombo vya habari kuandika siku hiyo ambayo ni ya kuzaliwa kwake, lakini pia atamsapraizi Wema.

 Club Maisha ilikuwa na wakati mgumu, kwani idadi ya watu walioingia katika shoo hiyo ilikuwa kubwa na kadiri muda ulivyozidi kwenda ndivyo wadau walivyozidi kuingia ndani, wengi wakiwauliza waliotangulia kama Diamond ameshakitegua kitendawili cha sapraizi.

 Kabla ya Diamond kupanda jukwaani na kuonesha ‘sapraizi’ kama alivyoahidi, wasanii kutoka Jumba la Vipaji Tanzania (THT) Barnaba Elias na makomandoo kadhaa walipanda jukwaani kwa nyakati tofauti na kupiga shoo safi.

 Baadaye, Hemed Suleiman ‘PHD’ ambaye pia anang’ara kwenye muvi za Kibongo, alipanda jukwaani na kuwaonesha mashabiki kwamba yeye ni mkali, kisha aliposhuka Diamond akapanda.


MC wa shoo hiyo, Hemed Kavu ‘HK’ aliagiza keki imfuate Diamond jukwaani ambapo mashabiki walianza kumuimbia wimbo wa ‘Happy Birthday’ huku shamrashamra zikirindima ukumbi mzima kwa pongezi za msani huyo kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa ambapo
ametimiza miaka kadhaa.

 Mama mzazi wa Diamond, alikuwa wa kwanza kulishwa keki, akifuatiwa na Wema Sepetu. Wao walilishana kwa midomo hali iliyosababisha shangwe kubwa kuibuka ukumbini.

 Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, Diamond alimwaga machozi hadharani pale alipomlisha keki kaka yake, Romeo Jones ‘Rommy’ ambapo alisema, alimsaidia sana wakati alipoanza kufurukuta kwenye ‘game’.

 Aliyefuata baada ya hapo alikuwa Jacob Steven ‘JB’ aliyewawakilisha wasanii wote wa kiume wa tasnia ya filamu kabla ya diva wa muvi nchini, Aunt Ezekiel naye kula kwa niaba ya wote wa kike.


                            AMPA TUZO BOB JUNIOR, WAMALIZA BIFU
Kitu kingine kilichoifanya hafla hiyo kuwa ya kipekee ni tuzo za heshima alizoziandaa msanii huyo kwa ajili ya kuwapa watu muhimu ambao wamechangia kwa namna moja au nyingine mafanikio yake kimuziki ambapo prodyuza wake wa kwanza, Raheem Nhanji ‘Bob Junior’ alikuwa miongoni mwao.Aidha, baada ya kutoa tuzo kwa Bob Junior, Diamond aliutangazia umati kwamba, lile
bifu kati yao halipo tena.

 “Bob Junior ni ndugu yangu, rafiki yangu na prodyuza wangu wa kwanza. Natambua sana mchango wake na niseme ukweli kwamba bila yeye nisingeweza kufika hapa nilipo leo.

 “Mikwaruzano ni kitu cha kawaida, lakini sasa sina kinyongo naye. Mimi ni Rais wa Wasafi, hivyo ni msafi hadi moyoni. Watu wasisambaze umbeya, sina tatizo tena na Bob Junior,” alisema kisha wakakumbatiana, makofi yakapigwa, waa waa.

 Mama mzazi wa Diamond naye alipewa tuzo na mwanaye, ambapo msanii huyo alisema anatambua mchango wa mzazi wake huyo si tu katika muziki bali katika maisha yake kwa ujumla.


Wengine waliopata tuzo hiyo ni prodyuza wake wa kwanza kumtengenezea video aliyotokea Visual Lab anayekwenda kwa jina la Adam Juma ambaye hakuwepo ukumbini, hivyo kupokelewa na Hamza wa THT kwa niaba yake.
Meneja wake wa kwanza kabisa aliyewahi kukwaruzana naye, Msafiri Peter ‘Papaa Misifa’ naye alipewa tuzo na Diamond kutangaza kwamba bila yeye (Papaa Misifa) asingefikia
mafanikio aliyonayo leo.

 Alisema: “Huyu amenitoa kuanzia mwanzo kabisa wakati naanza na singo ya Mbagala, bila msaada wake nisingetoka. Nathamini sana mchango wake.”

Mwisho aliwapatia tuzo madensa wa kundi lake kwa kumvumilia kuanzia walipoanza naye kazi kwa malipo madogo hadi sasa mambo safi na anawalipa vizuri.
Baada ya tendo hilo, Diamond alishuka jukwaani kumpisha Rashid Makwilo ‘Chid Benz’ ambaye alikamua shoo ya kufa mtu iliyomfanya ashangiliwe na mashabiki waliofurika ndani
ya ukumbi huo.


                                                SASA WEMA AVALISHWA PETE

Muda ukiwa umeyoyoma kabisa, mishale ya saa 9:37 usiku, Chid Benz aliposhuka madensa wa Diamond walipanda jukwaani peke yao na kucheza wimbo wa ‘Happy Birthday’ ikiwa ni ‘dedication’ kwa bosi wao huyo.
Baadaye kidogo, Diamond naye akapanda na kuangusha shoo ya kukata na shoka, lakini alikatisha na kuomba radhi akisema kuwa muda muafaka wa kuonesha ‘sapraizi’ aliyomuandalia Wema ulikuwa umefika.

 Wema akiwa na wasiwasi mwingi, akionekana kutokujua kitakachotokea, aliitwa jukwaani, akatembea kwa mwendo wa ‘sijui anataka kufanyaje?’ hadi alipomkaribia Diamond aliyekuwa amesimama akimwangalia.

 Wakiwa jukwaani, wadau walionesha kusubiri kwa hamu kauli ya Diamond, ndipo promota wake Hussein Ally alipanda na kumkabidhi msanii huyo pete ya dhahabu yenye ‘kijicho’ cha almasi sehemu ya juu ambapo naye bila kuchelewa alimvisha Wema kwenye kidole cha uchumba.

 Ilikuwa ni furaha kubwa sana kwa Wema aliyeonekana kuchanganyikiwa na kutoamini macho yake kwa vile hakutegemea kama ‘sapraizi’ aliyoahidiwa ingekuwa ni pete ya uchumba.


                                             DIAMOND AFUNGUKA
“Mengi yanasemwa, lakini nataka kuwaambia kwamba hakuna lenye mwanzo likakosa mwisho. Leo namhalalisha rasmi Wema kuwa mchumba wangu. Ndiye wangu wa maisha.”

 Wema aliduwazwa na tendo hilo, akabaki na tabasamu la kujilazimisha huku akiwaonesha mashabiki pete aliyovishwa.

 Kwa muda wa dakika mbili nzima, Wema na Diamond walikumbatiana kabla ya kuachana kisha staa huyo akawaongezea mashabiki mzuka kwa kupiga kibao cha Moyo Wangu.

 Diamond aliposhuka jukwaani, kundi la Tip Top Connection lilipanda kuonesha makali yake. Hadi paparazi wetu anajiondoa ukumbini humo, washikaji hao wa Manzese walikuwa bado wanaendelea kupagawisha.

 Tunawatakia heri na baraka tele Wema na Diamond katika safari yao ya kuelekea kwenye ndoa. Wawe waaminifu na wavumiliane kwenye matatizo ili mwisho wa pete yao uwe ni ndoa.









No comments:

Post a Comment