Dar es Salaam. Harakati za kuwania urais ndani
ya CCM zimeingia katika hatua mpya baada ya mwanasiasa mkongwe, Kingunge
Ngombale - Mwiru kuibuka na kudai kuwa wote waliojitokeza kuwania
nafasi hiyo hawana sifa kwa kuwa wanatumia fedha kutaka kuingia Ikulu.
Kauli ya mwanasiasa huyo ambayo imekuja siku moja
kabla ya Kamati Kuu ya CCM kukutana leo mjini Unguja na moja ya ajenda
ikitajwa kuwa suala la maadili, inaweza kuwa mwiba mchungu kwa wanasiasa
hao ambao wanaongezeka kila kukicha.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kingunge alisema:
“Kuna suala la kukosa uadilifu, kuna suala la matumizi ya pesa na
nikwambie ukweli, hao
wanaotangaza urais wote wanatumia pesa, wanatumia faulo mbalimbali na wananchi wanajua.”
wanaotangaza urais wote wanatumia pesa, wanatumia faulo mbalimbali na wananchi wanajua.”
Kwa miezi kadhaa sasa, baadhi ya makada wa CCM
wamekuwa wakitajwa kufanya harakati kichinichini na wengine kushiriki
shughuli za wazi zinazoashiria kuwa wanataka kuwania nafasi hiyo ya juu.
Hadi sasa makada wanne tayari wameweka wazi nia yao hiyo.
Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba kwa nyakati tofauti walitoa kauli
zinazowashutumu makada wengine wa chama hicho kwa matumizi makubwa ya
fedha katika kushawishi uungwaji mkono.
Hata hivyo, kauli za wanasiasa hao zimedaiwa kuwa
ni fitina za kisiasa kwa kuwa wagombea wote wanatoa fedha, bali
wanazidiana viwango tu.
Mbali na Makamba na Membe, wanaCCM wengine
waliotangaza au kutajwa kuwania urais ni Mbunge wa Nzega, Dk Khamis
Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda.
Wengine ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward
Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Stephen Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini,
William Ngeleja.
Kauli ya Kingunge aliyoitoa kupitia Televisheni ya
ITV, imekuja wakati wanasiasa sita miongoni mwa hao wanaotajwa
wakikaribia kumaliza miezi 12 ya uangalizi kutokana na onyo kali dhidi
yao lililotolewa na Kamati Kuu ya CCM Februari 18, mwaka jana baada ya
kuwatia hatiani kwa makosa ya “kuanza kampeni mapema na kufanya mambo
ambayo ni kinyume na maadili ya chama na ya jamii.”
Wanaotumikia adhabu hiyo ni Lowassa, Sumaye, Njeleja, Makamba, Wasira na Membe.
Akisisitiza hoja yake hiyo bila kutaja majina,
Kingunge alisema makada hao wamekuwa wakitumia fedha nyingi kujitangaza
na kutengeneza ushawishi wa kukubalika kwa wananchi jambo ambalo ni
kinyume na maadili ya uongozi.
Kingunge alisema mwanasiasa yeyote anayehitaji uongozi hapaswi kutumia fedha kushawishi wananchi wamchague.
- Mwananchi
- Mwananchi
No comments:
Post a Comment