Pages

Wednesday, October 12, 2011

MAMA MARIA NYERERE AWATAKA VIONGOZI KUWAJIBIKA ILI KUWALETEA MAENDELEO WATANZANIA







MJANE wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere amewataka Viongozi Serikalini kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuharakisha mchakato wa maendeleo kwa wananchi wake.
Ameyasema hayo leo wakati alipokutana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara na Viongozi waandamizi wa Wizara hiyo waliokwenda kumtembelea nyumbani kwake kijijini Butiama, mkoani Mara.
 Amesema ili wananchi wajenge imani na Serikali yao ni wajibu wa kila kiongozi katika eneo lake la kazi kuzingatia maadili ya kazi ambayo ndio msingi mkubwa wa maendeleo ya taifa lolote ulimwenguni.
“Leo hii wapo watu wanaolalamika kuwa Serikali haikufanya jambo lolote katika miaka 50 ya Uhuru, hiyo isiwape hofu kinachotakiwa sasa ni kwa kila kiongozi kuelewa kuwa anawajibika kufanya kazi aliyotumwa na wananchi waliomweka madarakani” Alisema Mama Maria.
Kwa mujibu wa Mama Maria amesema wakati Tanzania ikikaribia kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wake,kila Mtanzania anatakiwa kujiuliza tulipotoka na tunapokwenda kwa kuwa yapo maendeleo ya wazi yaliyopatikana katika kipindi hiki pamoja na baadhi ya makundi ya watu wachache kukosoa mafaniko hayo.
Aidha, Mama Maria amesema kuwa Wizara hii ni Wizara nyeti kwa kuwa inasimamia Sekta za Habari, vijana, Utamaduni na Michezo, hivyo ujenzi wa maadili na malezi hayana budi kusimamiwa kikamilifu ili taifa liweze kuwa na vijana wazalendo wenye lengo la kujenga taifa lao.
Aidha amesema suala la maadili yanajengwa kuanzia ngazi ya familia, shuleni na baadaye katika ngazi ya taifa, hivyo ni wajibu wa kila mzazi kumlea mtoto wake katika malezi bora yenye kuzingatia elimu, pamoja na uhakika wa chakula.
 Akifafanua zaidi amesema iwapo kila mzazi, kiongozi na mwananchi atatimiza wajibu wake upo uwezekano wa kupunguza manung’uniko ya wananchi kwa Serikali juu ya uwezo wake wa kiutendaji katika utoaji wa huduma za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
 Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt Fenella Mukangara amesema suala la maadili ni miongoni mwa masuala ya kimsingi yanayopewa kipaumbele na Wizara yake.
 “Wizara yangu ipo mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa inawajengea vijana uwezo wa kujitegemea na kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya taifa”
 Ameongeza kuwa Wizara yake pia inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa sekta ya michezo inaimarishwa na kuendelezwa ili kuleta amani na furaha kwa Watanzania.
 “Kuhusu habari, hapa kuna changamoto ikiwemo suala la maadili ya uandishi lakini hata hivyo Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha maandalizi ya sheria ya kusimamia vyombo vya habari” alisema Dkt. Fenella.
 Mbali na kumsalimia Mjane huyo, Viongozi hao pia walipata fursa ya kutembelea kaburi la Mwasisi wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na kupata historia fupi ya familia hiyo.
 Ziara ya Viongozi hao imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa Wizara hiyo, ambapo sherehe zake zinaendelea katika uwanja wa kumbukumbu ya Joseph Kazurira Nyerere, Butiama mkoani Mara.

No comments:

Post a Comment