MJANE
wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere
amewataka Viongozi Serikalini kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili
kuharakisha mchakato wa maendeleo kwa wananchi wake.
Ameyasema
hayo leo wakati alipokutana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara na Viongozi waandamizi wa
Wizara hiyo waliokwenda kumtembelea nyumbani kwake kijijini Butiama,
mkoani Mara.
Amesema
ili wananchi wajenge imani na Serikali yao ni wajibu wa kila kiongozi
katika eneo lake la kazi kuzingatia maadili ya kazi ambayo ndio msingi
mkubwa wa maendeleo ya taifa lolote ulimwenguni.
“Leo
hii wapo watu wanaolalamika kuwa Serikali haikufanya jambo lolote
katika miaka 50 ya Uhuru, hiyo isiwape hofu kinachotakiwa sasa ni kwa
kila kiongozi kuelewa kuwa anawajibika kufanya kazi aliyotumwa na
wananchi waliomweka madarakani” Alisema Mama Maria.
Kwa
mujibu wa Mama Maria amesema wakati Tanzania ikikaribia kuadhimisha
miaka 50 ya Uhuru wake,kila Mtanzania anatakiwa kujiuliza tulipotoka na
tunapokwenda kwa kuwa yapo maendeleo ya wazi yaliyopatikana katika
kipindi hiki pamoja na baadhi ya makundi ya watu wachache kukosoa
mafaniko hayo.
Aidha,
Mama Maria amesema kuwa Wizara hii ni Wizara nyeti kwa kuwa inasimamia
Sekta za Habari, vijana, Utamaduni na Michezo, hivyo ujenzi wa maadili
na malezi hayana budi kusimamiwa kikamilifu ili taifa liweze kuwa na vijana wazalendo wenye lengo la kujenga taifa lao.
Aidha
amesema suala la maadili yanajengwa kuanzia ngazi ya familia, shuleni
na baadaye katika ngazi ya taifa, hivyo ni wajibu wa kila mzazi kumlea
mtoto wake katika malezi bora yenye kuzingatia elimu, pamoja na uhakika
wa chakula.
Akifafanua
zaidi amesema iwapo kila mzazi, kiongozi na mwananchi atatimiza wajibu
wake upo uwezekano wa kupunguza manung’uniko ya wananchi kwa Serikali
juu ya uwezo wake wa kiutendaji katika utoaji wa huduma za kijamii,
kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt
Fenella Mukangara amesema suala la maadili ni miongoni mwa masuala ya
kimsingi yanayopewa kipaumbele na Wizara yake.
“Wizara
yangu ipo mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa inawajengea vijana
uwezo wa kujitegemea na kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya taifa”
Ameongeza
kuwa Wizara yake pia inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa
sekta ya michezo inaimarishwa na kuendelezwa ili kuleta amani na furaha
kwa Watanzania.
“Kuhusu
habari, hapa kuna changamoto ikiwemo suala la maadili ya uandishi
lakini hata hivyo Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha
maandalizi ya sheria ya kusimamia vyombo vya habari” alisema Dkt.
Fenella.
Mbali
na kumsalimia Mjane huyo, Viongozi hao pia walipata fursa ya kutembelea
kaburi la Mwasisi wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere
pamoja na kupata historia fupi ya familia hiyo.
Ziara
ya Viongozi hao imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50
ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa Wizara hiyo, ambapo sherehe zake
zinaendelea katika uwanja wa kumbukumbu ya Joseph Kazurira Nyerere,
Butiama mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment