Pages

Friday, October 21, 2011

NICO NYAGAWA MENEJA MPYA WA SIMBA SC



Uongozi wa klabu ya Simba umemteua, nahodha wake wa zamani, Nico Nyagawa, kuwa meneja mpya wa timu hiyo inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Nyagawa ambaye aliachwa katika usajili wa msimu huu, aliahidiwa kupewa ajira nyingine kutokana na mkataba wake kuendelea kuwepo na alikaa kimya tofauti na wachezaji wenzake ambao walipewa taarifa za kutemwa katika kipindi ambacho hawakuwa na nafasi ya kufanya mazungumzo na klabu nyingine.
Kiungo huyo ambaye alisajiliwa Simba mwaka 2005 akitokea Mtibwa Sugar ya Turiani, Manungu mkoani Morogoro, alianza kazi yake hiyo mpya jana asubuhi na alipewa mikoba hiyo baada ya aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo, Abdallah Kibaden 'King' kuwa safarini kwenye ibada ya Hijja mjini Makka.
Akizungumza na blog hii jana mchana, Nyagawa alithibitisha kurejea kundini na kuahidi kutumia uzoefu aliokuwa nao kuisaidia Simba ili ifikie malengo yake.
"Ni kweli nimeitwa na nitaanza kazi rasmi leo (jana) jioni," alisema Nyagawa ambaye msimu huohuo wa mwaka 2005/2006, Simba ikitumia uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, aliifungia mabao mawili katika mchezo uliomalizika kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga.
Wekundu wa Msimbazi hawakuwa na meneja wa kudumu tangu Innocent Njovu alipoondolewa baada ya mabadiliko yaliyofanywa na uongozi wa sasa wa Simba kufuatia kuondoka kwa kocha Mzambia, Patrick Phiri.
Nyagawa anatarajiwa kuwa kwenye benchi la ufundi la timu hiyo kwa mara ya kwanza kesho wakati watakapoivaa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba wanaongoza kwenye msimamo wa ligi ya Bara baada ya kushuka dimbani mara 10 na kufikisha pointi 24 huku wakifuatiwa na ‘maafande’ JKT Oljoro waliocheza mechi za idadi sawa na Simba na kufikisha pointi 19.

No comments:

Post a Comment