Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, October 6, 2011

Simba yawapiga stop Boban, Yondani













UONGOZI wa Simba umewasimamisha wachezaji Haruna Moshi 'Boban' na Kelvin Yondani kutokana na kuchoshwa na vitendo vyao vya utovu wa nidhamu.

Habari za ndani ambazo Mwananchi imezipata zinasema Moshi na Yondan tayari wameshaandikiwa barua ya kusimamishwa kwa madai wachezaji hao wamekuwa wakijiona kuwa ni bora zaidi na hawaudhurii mazoezini.

"Boban anajiona yeye ni staa zaidi hajatokea na wala hajapangwa mechi ya Mtibwa, Polisi Dodoma, Kagera Sugar kwa sababu hafanyi mazoezi, hakuna 'Super Star Simba' njoo mazoezini utapangwa, hata hivyo uongozi umechoshwa na tabia zake umeamua kumfungashia virago,"kilidai chanzo hicho.

Mbali na Boban ambaye alikatisha mkataba wake na timu ya Gefle IF ya nchini Sweden, pia Simba imemfungashia virago beki wake Yondani ambaye hajaonekana kwenye mazoezi tangu mechi yao na Kagera Sugar na ile ya Toto African iliyofanyika mkoani Mwanza.

Chanzo hicho cha habari kimeeleza kuwa tayari wachezaji hao wameshaandikiwa barua za kutimuliwa ndani ya klabu hiyo.

Simba inayofundishwa na Mganda Moses Basena itawajadili wachezaji, Emmanuel Okwi na Ulimboka Mwakingwe walioshindwa kufanya mazoezi na timu hiyo tangu Jumatatu.

Katika hatua nyingine chanzo hicho kilidai kuwa Okwi aliyeachwa kwenye kikosi cha Uganda hajatokea mazoezini kwa kisingizio kuwa anaumwa malaria, lakini uongozi umebaini haumwi, mwenzake Ulimboka alidai amefiwa na baba yake mdogo.

"Kilichopo hapo ni kwamba Ulimboka umri umeenda sasa hivi mazoezi wanayofanya ni ya nguvu zaidi na sio chini ya masaa matatu, sasa Ulimboka anaogopa si mnakumbuka Zanzibar alichanika nyama ya paja kwa sababu ya mazoezi magumu, hivyo anavuta vuta mpaka ikifika mazoezi mepesi ndio aje, hakuna cha msiba wala nini,"alidai kiongozi huyo kwa sharti la kutotajwa jina.

"Kwa upande wa Okwi safari hii hajaitwa timu ya Taifa, yupo hapo Chang'ombe anajifanya anaumwa hana cha kuumwa wala nini tumeshawaandikia barua wote kuwaambia wajieleze ni kwa nini tusiwape adhabu,"alisisitiza na kuongeza.

"Sasa hivi mwalimu anachofanya Simba kubwa mazoezi wanafanya na timu B lengo ni kuwapa nafasi zaidi timu B ili akija fanya mabadiliko watu wasishangae wala kulaumu, hatuwezi fuga maradhi kila siku, mwisho wa siku yatakuja kutuua.

Akizungumzia suala hilo msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema,"Taarifa za wachezaji wote tunazo na tunashughulikia masuala yao,"alisema bila ya kufafanua.

No comments:

Post a Comment