Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, October 11, 2011

WANANCHI WACHOMA MOTO NYUMBA YA JAMBAZI ,














 Moto ukiteketeza nyumba iliyokuwa ikitumika kuhifadhi mali za wizi













Meya wa manispaa ya Iringa Aman Mwamwindi (katikati) akitoa maagizo ya kuvunjwa kwa nyumba ya jambazi huyo baada ya nyumba hiyo kuwa na alama za X













 Watuhumiwa wa ujambazi wakiwa chini ya ulinzi wa polisi













 Mwananchi akiiba mahindi ya jambazi huyo,baada ya mali zake kuchomwa moto













Wananchi wakitazama mali mbali mbali zikiteketea kwa moto baada ya kuamua kuchoma moto kama njia ya kumwamisha jambazi huyo katika mtaa













WANANCHI wa Manispaa ya Iringa wafanikiwa kuvunja na kuteketeza kwa moto nyumba Msafiri Ilomo ambayo ilikuwa ikitumika kama ngome ya ujambazi katika eneo la Kigamboni kata ya Mwangata na kufanikiwa kukuta mali mbali mbali ambazo wananchi walikuwa wakiporwa kabla ya kupigwa nondo .

Pamoja na wananchi hao kuteketeza kwa moto nyumba hiyo na mali mbali mbali zinazodaiwa kuwa ni za wizi bado baadhi yao walionyesha kuiba baadhi ya mali hizo za wizi zilizokuwa zikimilikiwa na jambazi huyo.

Hatua ya wananchi hao kuvunja nyumba hiyo ilikuja baada ya mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi kufika eneo hilo na kushuhudia wingi wa mali zilizoporwa kwa wananchi zikiwemo mali za baadhi ya wananchi ambao waliuwawa kwa kupigwa nodo na majambazi hao.

Kabla ya Mwamwindi kukubali ombi la wananchi hao la kutaja nyumba hiyo kuvunjwa katika eneo hilo tayari jeshi la polisi lilifika eneo hilo na kusomba mali mbali mbali kwa zaidi ya tripo mbili na kwenda kuzihifadhi kituo cha polisi kwa ajili ya utambuzi zaidi .

Akizungumza na wananchi hao Mwamwindi alisema kuwa kutokana na nyumba hiyo kuwa na alama ya X kutokana na kujengwa bila ruhusa ya ofisi ya Manispaa ya Iringa anaagiza baada ya jeshi la polisi kumaliza kazi yao nyumba hiyo kuvunjwa .

Meya huyo alisema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa juu ya tukio hilo la ujambazi katika kata ya Mwangata ambapo wananchi walikuwa wakiishi kwa hofu kubwa na tayari watu zaidi ya wawili wamepoteza maisha kwa kupigwa nondo huku baadhi ya wanawake wamebakwa na kundi hilo la ujambazi lililokuwa na masikani yake Kigamboni katika nyumba ya jambazi huyo Ilomo.

Baadhi ya majeruhi waliopigwa nondo na kukatwa mapanga na kundi hilo la ujambazi akiwemo Michael Chengula (37) aliyevunjwa mkono wake wa kushoto kabla ya kuporwa simu na fedha kiasi cha laki moja na Adilian Lusasi (45) ambaye ni mpiga picha aliyeporwa kamera na picha za wateja wake walisema kuwa walivamiwa na jambazi huyo na kundi lake majira ya saa 3 za usiku zaidi ya wiki tatru zilizopita.

Pia walisema tayari kijana Damas Kisinga amepoteza maisha kwa kupigwa nondo na kundi hilo la ujambazi na kuzikwa juzi katika eneo la Makanyagio huku nyumba ya diwani wa kata ya Mkwawa Thobias Kikula ikivamiwa na wezi hao ambao walishindwa kufanikiwa baada ya kuzingirwa na wananchi .

Diwani wa kata ya Mwangata Galus Lugenge akielezea mali zilizokamatwa alisema kuwa ni pamoja na TV, DVD, nguo, vyombo ,Magodoro , Baiskeli, sofa ,masanduku ya nguo , vitanda , mabati na simu aina ,visu , CD , vyombo vya makanisani na misikitini na mali nyingine nyingi ambazo zilijaa nyumba na kusombwa na magari ya polisi.

Alisema kuwa mwezi mmoja uliopita jambazi huyo alifiwa na motto wake na kulazimika kuzika kwa siri na msiba kutenga nyumbani kwa mzazi wake akihofu wananchi kujua siri nzito katika nyumba hiyo kuu kuu (Pagale).

Diwani Lugenge alisema kuwa nyumba hiyo ilikuwa haijakamilika japo ilifunikwa kwa trubai pekee na nje alikuwa amefunga dishi la kawaida na la DSTV jambo mbalo liliwafanya wananchi kuishuku nyumba hiyo na kuivamia kabla ya jambazi hilo kufanikiwa kuwatoroka.

"Jana tulianza msako baada ya kijana mmoja kunusurika kukatwa nondo na baada ya kupiga kelele wananchi walitoka na kuanza kumfukuza jambazi huyo na wenzake ambao walikuwa wakielekea katika nyumba hiyo .....yaani baada ya kufika hatukuamini baada ya kukuta mbwa wakila chakula kwa kutumia Hotipoti za gharama kubwa huku mali zikiwa zimejazana ndani ya nyumba mali zinazokadiliwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 15"Alisema jambazi huyo aliweza kuwatoroka kwa kuruka ukuta

Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi walidai kuwa jambazi huyo alikuwa ametolewa jela kwa msamaha wa Rais na kuwa tayari amefanya unyama wa kutisha katika mji wa Iringa kuwa katika mali hizo begi la mwanafunzi wa sekondari

Wakati huo huo watu wawili wamenusurika kuuwawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kukamatwa wakiiba mali za jambazi huyo ambazo zilipaswa kuteketezwa kwa moto.


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu alisema kuwa yupo nje ya mkoa ila taarifa za tukio hilo amepata na kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na jeshi la polisi huku akiwataka kuendelea kuwafichua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uharifu

No comments:

Post a Comment