Pinda:Hata wanyama hawafanyi ushoga |
Kizitto Noya, Dodoma
WAZIRI
Mkuu Mizengo Pinda amezungumzia sakata la Uingereza kutishia kuinyima
misaada Tanzania kama haitaruhusu ndoa za jinsia moja, akisema,
"haiwezekani, kwa kuwa hata wanyama hawafanyi hivyo."
Alisema
kama ilivyoelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, Tanzania ipo tayari kukosa misaada ya
Uingereza iwapo kigezo cha kupata misaada hiyo, ni nchi kuruhusu ndoa za
jinsia moja.
Waziri Mkuu Pinda alitoa kauli
hiyo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu
Chadema, Regia Mtema katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa
Waziri Mkuu.
Katika swali lake hilo, Mtema
alitaka kusikia kauli ya Serikali kuhusu msimamo huo wa Uingereza
uliotolewa na Waziri wake Mkuu David Cameroon na kujua endapo Tanzania
imeshaanza kujipanga kuikataa misaada ya nchi hiyo.
“Mheshimiwa
Waziri Mkuu, hivi karibuni tumesikia Waziri Mkuu wa Uingereza David
Cameroon akisema ili tupate misaada yao, tukubaliane na suala la ndoa za
jinsia moja. Nini kauli ya Serikali? Je kama taifa, tumeshaanza
kujipanga kuikataa misaada hiyo?,”alihoji Mtema.
Akijibu
swali hilo Pinda alisema,"Kauli ya Serikali ilishatolewa na Waziri
Membe mwenye dhamana na kurudiwa mara kadhaa na mawaziri wengine. Mimi
sina kauli nyingine labda nitoe maoni yangu tu.”
Aliongeza; “Niseme tu kuwa mimi nakubaliana na msimamo huo wa Tanzania kwani, hata wanyama hawafanyi hivyo.”
Kauli
ya Waziri Mkuu Pinda imekuja wiki chache tangu Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alipotoa msimamo wa Serikali
kuhusu suala hilo, ambapo alisema kwamba Tanzania ipo tayari kukosa
misaada yote kutoka Serikali ya Uingereza na kamwe haiwezi kuruhusu
sheria inayotambua mashoga na kuhalalisha ndoa za jinsia moja.
Msimamo
huo mzito wa Serikali umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa
Uingereza, David Cameron, kutamka kwamba nchi yake ina mpango wa
kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria na katiba zao, hazitambui
mashoga na ndoa za jinsia moja.
Cameron
alikaririwa akithibitisha kuwa tayari amewajulisha juu ya suala hilo
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola waliokuwa wakihudhuria
mkutano wa Jumuiya hiyo uliomalizika siku nne zilizopita, mjini Perth,
Austaralia ambao pia ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete.
Waziri
Mkuu huyo kutoka chama cha Conservative ambacho kilishinda uchaguzi Mei
mwaka jana, alisema suala hilo la mashoga na ndoa za jinsia moja, ni
moja ya mambo yanayoongoza sera ya Serikali yake kuhusu misaada kwa
mataifa mbalimbali na kwamba tayari imeanza kutekelezwa katika maeneo
kadhaa duniani.
Kauli ya Cameron imechukuliwa
kama kielelezo cha ukoloni mamboleo ambao Uingereza inajaribu
kuupandisha daraja kwa mataifa yanayoendelea kwa kigezo cha misaada.
Lakini, Waziri Membe alisema pamoja na umasikini wake, Tanzania kamwe haitaruhusu upuuzi huo kwa kigezo cha misaada.
“
Tanzania ni nchi maskini, lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti
kwa sababu ya misaada na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni wetu,
hata sheria zetu zinakataa,” alisema Membe.
Alifafanua
kuwa katika kuonesha msimamo wa kutokukubaliana na masharti hayo,
Tanzania imeshikilia msimamo thabiti kupinga upuuzi huo ambapo Januari
mwaka huu, ilimkataa balozi shoga ambaye aliteuliwa na nchi yake kuja
kuiwakilisha hapa nchini. Hata hivyo Waziri Membe hakutaja jina la
balozi huyo wala nchi anayotoka.
“Niwape siri
moja ambayo tuliificha lakini leo ngoja niwaambie, mwanzoni mwa mwaka
jana nililetewa barua kunijulisha ujio wa balozi mmoja anayekuja
kuiwakilisha nchi yake, mwanamume mwenye ndoa ya jinsia moja. Nilikwenda
kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuhusu wasifu wa balozi huyo mtarajiwa
naye akajibu kwa maneno matatu, yarabi toba! Mkatae!,”alisema Membe.
Waziri
Membe alifafanua kuwa serikali ilimkataa balozi huyo kwa kuwa ni
kinyume cha utamaduni wetu na sheria za nchi kuwa na watu wenye tabia
hizo.
Alisema alimjulisha Waziri wa Mambo ya
Nje wa nchi hiyo kwamba balozi huyo haruhusiwi kuja kufanya kazi nchini
kwa kuwa ni kinyume na utamaduni wetu. “Waliendelea kuniomba kwamba
balozi huyo akija hatatoka kwenye makazi yake akiwa na mwenza wake hivyo
watu hawatamuona lakini tulimkataa kabisa, wakatuelewa.”
Alieleza
kuwa tamko hilo la Waziri Mkuu Cameron linaweza kusababisha hatari ya
kuvunjika kwa uhusiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola
na koloni mama Uingereza na waziri huyo atabeba lawama hizo.
Kwa
mujibu wa Waziri Membe Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha tisa,
kinatambua ndoa ya jinsia mbili tofauti, yaani mume na mke.
“Sheria
hizi tunazozitumia hivi sasa tumezirithi kutoka Uingereza ambako leo
wanatukuza ndoa za jinsia moja na ushoga,” alisema Membe.
Suala
la kile kinachoitwa haki za binadamu kuhusu ushoga ilikuwa moja ya
ajenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana katika mkutano
Perth. Hoja ya kukomesha vizuizi dhidi ya ushoga na ndoa za jinsi moja
lilikuwa moja ya mapendekezo yaliyokuwamo katika ripoti ya ndani kuhusu
matarajio ya baadaye ya Jumuiya hiyo ya Madola.
|
No comments:
Post a Comment