Pages

Wednesday, December 14, 2011

Rais Jammeh kutawala kwa miaka 'bilioni'


Rais Jammeh asema ataongoza kwa miaka bilioni moja
Rais wa Gambia Yahya Jammeh ameambia BBC kwamba ataongoza kwa miaka "bilioni moja", kama Mungu akipenda.
Anasema wale wanaomkosoa na kumshutumu kuwa alishinda uchaguzi wa mwezi uliopita kwa kutumia vitisho na ufisadi "wanapoteza muda wao".

Shirika la Afrika Magharibi Ecowas lilisema kuwa wapiga kura "walitishwa".
Bwana Jammeh, aliyeingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1994, alichaguliwa tena kwa asilimia 72, hiyo ni kwa mujibu wa takwimu rasmi.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 46 anasema haogopi kile kilichomtokea Rais aliyeondolewa madarakani wa Misri Hosni Mubarak au Muammar Gaddafi wa Libya ambaye aliuawa.
"hatima yangu iko mikononi mwa mwenyezi Mungu," alimwambia mwandishi wa BBC.

"Nitawatimizia raia wa Gambia na kama nitatawala nchi hii kwa miaka bilioni moja,nitafanya hivyo, Mungu akipenda."
Uchaguzi wa mwezi Novemba ulikuwa wa nne tangu Bwana Jammeh alipompindua rais wa kwanza aliyeingia madarakani wakati nchi hiyo ilipopata uhuru Dawda Jawara akiwa na umri wa miaka 29.

Wagombea wa upinzani Ousainou Darboe na Hamat Bah walipata asilimia 17 na 11 mtawalia.
Bwana Darboe aliyataja matokeo hayo kama "yasiyo halali, ya kifisadi na ya kipuuzi".

No comments:

Post a Comment