Pages

Tuesday, February 7, 2012

Msanii aliyekufa 'afufuka' Afrika Kusini

Afrika Kusini
Kizazaa chazuka Afrika Kusini
Mtu mmoja nchini Afrika Kusini anayedai kuwa ni mwanamuziki mashuhuri aliyekufa, anashikiliwa na mamlaka za nchi hiyo hadi watakapothibitisha utambulisho wake kwa vipimo vya DNA, wamesema polisi.
Mtu huyo anasema yeye ni Khulekani "Mgqumeni" Khumalo - mwanamuziki wa nyimbo za kiasili za Kizulu ambaye alifariki mwaka 2009.

Anadanganya?

Hata hivyo alizuka katika nyumba ya familia yake wiki iliyopita akidai kuwa alikuwa ametekwa na mizuka.
Familia yake wakiwemo wake zake wawili, wanasema anaonekana kuwa ndio mwenyewe - lakini polisi wamesema atashtakiwa kwa udanganyifu iwapo vipimo vya DNA vitaonesha anadanganya.
Mwandishi wa BBC mjini Johannesburg, Nomsa Maseko amesema polisi wanatarajia kupata majibu ya vipimo vya DNA baadaye wiki hii - na mpaka wakati huo mtu huyo atasalia kizuizini.

Mashabiki

Mwandishi wetu anasema iwapo vipimo vya DNA vitaonesha kweli ni Bw Khumalo, polisi watalazimika kwenda mahakamani kupata kibali cha kufukua maiti, ili kujua nani hasa alizikwa, katika mazishi yaliyokuwa ya hali ya juu ya Bw Khumalo ambayo yalihudhuriwa na wanasiasa, vyombo vya habari na mashabiki wake.
Mwandishi wetu anasema kesi hiyo imezua kizazaa nchini Afrika Kusini - na siku ya Jumapili iliyopita, maelfu ya mashabiki walikwenda Kwazulu-Natal kushuhudia "kutolewa" rasmi kwa mtu huyo.
Polisi walitumia maji yenye nguvu kutawanya watu baada ya msongamano kutokea kutokana na kila mtu kutaka kumuona mtu anayejiita Bw Khumalo.

Upelelezi

Akitumia kisemeo, aliwaambia mashabiki wake kuwa hakuwa amekufa - lakini alipotea baada ya kuchukuliwa na wachawi.
Amesema alifungiwa katika pango na mizimu kwa miaka miwili, na alilazimishwa kuimba na kulazimika kula matope ili asife kwa njaa.
"Nimekuwa hai muda wote," amekaririwa akisema na gazeti la The Times la Afrika Kusini.
"Nimepoteza uzito mwingi lakini ni mimi," alisema.
Mtu huyo, ambaye hakuwa na mtindo wa nywele wa rasta ambao Bw Khumalo alikuwa nao, alipuuza ombi la mashabiki la kumtaka aimbe, badala yake alitaja majina ya ukoo wake, kwa mujibu wa gazeti la The Times.
Polisi wa Afrika Kusini wamesema wanashughulikia mkasa huo kwa kufanya upelelezi wa kesi ya uhalifu.

No comments:

Post a Comment