Viongozi
wanaopenda matanuzi katika magari ya kifahari ya serikali sasa ukomo
umefika baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuzuia vibali vya ununuzi wa
mashangingi ambapo wakurugenzi wote waliopo katika ofisi yake wameanza
kutumia magari aina ya RAV4 ukiwa ni mkakati wa kubana matumizi ya
Serikali.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi,
alisema hayo wakati akihojiwa na kituo cha Televisheni cha ITV katika
kipindi cha dakika 45.
Alisema
Serikali imeanza kutekeleza mpango wake wa kubana matumizi yasiyokuwa
ya msingi tangu Waziri Mkuu alipozuia vibali vya ununuzi wa mashangingi
na kama ni lazima kununua gari kinatolewa kibali cha kununua gari aina
ya Double Cabin au Hard Top.
“Gari
lenye gharama ya Sh. milioni 200 Waziri Mkuu amefuta ambapo kwa muda
mrefu sasa magari mengi yenye thamani kubwa hayanunuliwi, lakini pia
matumizi ya mafuta kwa ajili ya kurandaranda yamepungua sana,” alisema
Lukuvi.
Alimtolea
mfano Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba ameanza kutekeleza agizo
la serikali ambapo wakurugenzi wote wa ofisi hiyo wameanza kununua
magari ya RAV4 ambayo gharama yake ni pungufu ya asilimia 20 ya gharama
ya shangingi.
Lukuvi
alisema magari hayo ya kifahari yakishafikia kilometa 100 matengenezo
yake kwa mwezi yaweza kuwa karibu Sh. milioni 10 na yanapokuwa makongwe
matumizi yake yanakuwa gharama kubwa.
Aliongeza
kuwa serikali inatarajia kuona maofisa kuanzia wakurugenzi au makatibu
wakuu kila mmoja anaangalia mbinu na mikakati ya kupunguza gharama
kwenye sekta yake bila kusubiri kupewa maelekezo ili kuokoa fedha ambazo
zitapelekwa kwenye shughuli za maendeleo.
Lukuvi
alifafanua kuwa matarajio ya serikali ni kuona katibu mkuu na
mkurugenzi wanabana matumizi hadi kwenye halmashauri na kuwataka wakuu
wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa wawabane wakurugenzi ambao baadhi
yao wanasafiri sana nje ya vituo vyao vya kazi.
“Ukienda
kuchukua vitabu vya wageni unashangaa mkurugenzi hajaenda hata vijiji
viwili, lakini anatoka nje ya wilaya kila siku,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment