LICHA ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
kuwataka madaktari nchini kurejea katika meza ya mazungumzo, kwa maelezo
kuwa baadhi ya madai yao yameshughulikiwa, wataalamu hao wamemjibu
wakisisitiza kwamba mgomo wao upo pale pale kuanzia kesho.
Madaktari hao wamesema kuwa Waziri
Mkuu, amelidanganya Bunge jana wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo,
kwa kuesema kuwa kati ya madai yao kumi waliyowasilisha, matano
yameafikiwa na kila upande.
Kwa mujibu wa madaktari, wiki mbili
za mgogoro na serikali walizozitoa zinamalizika leo, hivyo kuanzia kesho
kada zote wanaingia katika mgomo usiokuwa na kikomo.
Majibu ya madaktari hao, yalitoka na
kauli ya Pinda bungeni jana wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani, Freeman Mbowe (CHADEMA), aliyetaka kujua malumbano kati ya
serikali, madaktari na walimu yatatatuliwa lini ili kuepusha mgomo.
Katika hilo, Pinda, alilieleza Bunge
kuwa tangu awali serikali iliunda kamati maalumu ya kushughulikia suala
hilo ambapo miongoni mwa madai yao kumi, matano yameafikiwa na kila
upande.
“Ninajua uzito wa hili jambo na
lilipotokea tulijitahidi kuhakikisha tunaunda kamati maalumu ili kuweza
kushughulikia masuala haya, na kwa mujibu wa kamati ni mambo matano kati
ya kumi, tumeafikiana kwa pamoja,” alisema na kuongeza kuwa:
“Baada ya hatua zote hizo kwa mujibu
wa sheria ni lazima makubaliano yao yasajiliwe na Tume ya Usuluhishi
(CMA), na kwamba hilo limefanyika ambapo tume ya serikali na upande wa
madaktari wamemaliza kazi yake.
“Hata hivyo mambo matano yaliyobaki,
nilimuagiza tena Waziri wa Afya awaandikie barua madaktari ili waweze
kukutana, lakini hadi juzi wanajibu barua ile wanasema hawazezi kukutana
tena na serikali kwa sababu haijatelekeza madai yao,” alisema Pinda.
Kwamba kati ya madai waliyotaka na
serikali imeyatekeleza ni pamoja na kuondolewa kwa mawaziri wa wizara
hiyo, kuongezwa posho ya kuitwa kazini, kufanya uchunguzi wa maiti na
nyinginezo.
“Lakini pamoja na hali hii serikali
ilifungua kesi ikilalamikia mgomo wa madaktari uliotokea mwanzoni mwa
mwaka huu, tume ya usuluhishi ilizitaka pande mbili, kamati ya serikali
na wawakilishi wa madaktari kukaa meza moja na kuzungumza Juni 19, mwaka
huu,” alisema.
Alifafanua kuwa mambo matano
waliyoafikiana ni serikali kukubali kuongeza posho ya kuitwa kazini
kutoka sh 10,000 hadi sh 15,000 kwa madaktari walio kwenye mafunzo
kazini na sh 20,000 kwa madaktari na sh 25,000 kwa madaktari bingwa.
“Pia serikali iliongeza posho ya
uchunguzi wa maiti kutoka sh 10,000 hadi 100,000 kwa madaktari na sh
50,000 kwa wasaidizi,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
Aliongeza kuwa serikali ilikubali
kuwapa kadi ya Bima ya Afya ya rangi ya kijani ambayo ina hadhi ya
huduma za daraja la kwanza kwa madaktari, pia kutoa chanjo ya ugonjwa wa
ini ambapo fedha za chanjo hiyo zimo kwenye bajeti ya mwaka ujao wa
fedha 2012/2013.
Hata hivyo, maelezo yake ylipingwa na
Chama cha Madaktari (MAT), ambapo kwa niaba yao, Mwenyekiti wa Jumuiya
ya wanataaluma hao, Dk. Steven Ulimboka, alisema kuwa hawako tayari
kupeleka suala hilo katika Mahakama ya Kazi kama alivyoeleza waziri
mkuu.
Alisema ni jambo la aibu kwa viongozi
wakuu wa serikali kuamua kwa makusudi kulidanganya Bunge wakati wakijua
wazi hakuna utekelezaji wa aina yoyote uliofanywa.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa katika
madai yote ya madaktari hakuna dai hata moja ambalo limetekelezwa kama
inavyoelezwa na viongozi.
Alisema kitu cha kushangaza hata taarifa ya ufafanuzi wa madai yao hakuna eneo ambalo serikali imeweka saini.
“Mgomo huu ni wa madaktari wa ngazi
zote nchini ambao hauna kikomo na tunachohitaji ni kuelezwa na serikali
hatua waliyofanya kuliko wanavyoendesha propaganda na kuweka siasa
katika madai yetu,” alisema.
Alisema pamoja na madai yaliyotolewa
na madaktari lakini kitu cha ajabu kilichofanywa na serikali ni kuamua
kuchomeka dai la posho ya uchunguzi wa maiti ambalo halijawahi kutolewa
na madaktari.
“Serikali inataka kutafuta ionekane
imetenda mema kwa madaktari kwa kudai kupandisha kima cha posho ya
uchunguzi wa maiti kutoka sh 10,000 hadi sh 100,000 wakati sisi
hatujawahi kuomba posho hiyo,” alisema.
Alisema posho hiyo si muhimu kwa
madaktari kwa kuwa wapo baadhi ya madaktari wanaoweza kufanya kazi kwa
zaidi ya miaka 30 bila kufanya uchunguzi huo.
Dk. Ulimboka alisema kuwa Watanzania
hawapaswi kuwalaumu madaktari kwa kuwa anayepaswa kubebeshwa lawama hizo
ni serikali iliyoshindwa kuboresha afya pamoja na kutatua migogoro.
Alisema walitegemea kwa siku 90
walizokaa katika meza ya majadiliano na kamati iliyoundwa na serikali
wangepata ufumbuzi wa madai yao, matokeo yake imekuwa ni matatizo zaidi.
“Kuhusu huduma za dharura katika maeneo nyeti watakaa na kutafuta ufumbuzi hapo baadaye,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Charles Misango na Danson Kaijage (Dodoma), Betty Kangonga na Chalila Kibuda (Dar).SOURCE UJANA TZ
No comments:
Post a Comment