Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, July 4, 2012

Balozi wa Tanzania Mjini Washington D.C Balozi Mwanaidi Sinare Maajar Aongoza Mabalozi Wawili wa Heshima wa Tanzania Katika Majimbo Mawili ya Marekani ya Minessota na San Francisco Kuonana na Makamu wa Pili wa Rais wa Znzibar Balozi Seif Ali Iddi


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mabalozi wa Heshima wa Tanzania katika baadhi ya Majimbo ya Marekani Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kulia yake ni Balozi wa Tanzania Washington D.C Bibi Mwanaidi Sinare, Bwana Kjell Berg Minessota na Bwana Ahmed Issa Alqassim San Francisco. Kushoto ya Balozi ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Slum Moh’d, Naibu wake Nd. Said Shaaban pamoja na Bwana Saleh ambae ni Msaidi wa Balozi Jimbo la Washington.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Znzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa zawadi kwa mmoja wa Wafanyabiashara Waandamizi waliounda Kundi la VIP Safari kutoka Nchini Marekani ambao wapo Nchini kuangalia uwezekano wa namna ya Kampuni zao kuwekeza Vitega Uchumi Nchini Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Alio Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa wa Wafanyabiashara waandamizi wa Kundi la VIP Safari baada ya kuwaandalia chakula cha usiku hapo Serena Inn Hoteli Shangani Mjini Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Balozi wa Tanzania Washington D.C Bibi Mwanaidi Sinare na Balozi wa Heshima MjiniMinessota Bw. Kjell Berg. Kushoto yake ni Waziri wa Hbari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk, Mke wa Balozi Seif Mama Asha Suleimana Iddi pamoja na Mmoja wa Wafanyabiashara hao wa VIP Safari.Picha na Saleh Masoud
---
Na Othman Khamis Ame
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Mazingira ya Kimaumbile yaliyoizunguuka Zanzibar bado yana fursa nzuri ya kutumiwa katika shughuli za Uwekezaji Vitega Uchumi. 

Balozi Seif alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Mabalozi wawili wa Heshima wa Tanzania katika majimbo mawili ya Marekani ya Minessota na San Francisco hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 

Mabalozi hao Bwana Ahmed Issa Qassim atakayeiwakilisha Tanzania katika Jimbo la San Francisco na Bwana Kjell Berg wa Jimbo la Minessota waliongozwa na Balozi wa Tanzania Mjini Washington D.C Balozi Mwanaidi Sinare Maajar. 
Balozi Seif alisema katika kuyatumia vyema mazingira hayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajaribu kuongeza nguvu za uimarishaji wa miundo mbinu katika Sekta ya Utalii. 

Alisema licha ya Sekta ya kilimo kuchukuwa nafasi kubwa ya Uchumi wa Taifa lakini eneo la utalii pia lina fursa nzuri ya kuwa muhimili wa Pili wa Uchumi wa Zanzibar kwa hivi sasa. 

Balozi Seif alifahamisha kwamba serikali inaangalia pia uwekezaji wa maeneo ya Kumbi za Mikutano ya Kiutalii kutokana na kupanuka zaidi kwa sekta hiyo hivi sasa. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaomba Mabalozi hao wa Heshima wa Tanzania katika Majimbo ya Marekani kuwa wawakilishi wazuri wa kuitangaza Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kwa wawekezaji kwenye majimbo watakayoyafanyia kazi. 

Balozi Serif aliwaahidi wawakilishi hao kwamba Serikali zote mbili zitajitahidi kutoa msaada kwao kwa vile kazi watakazokwenda kuzifanya ni kwa ajili ya Watanzania. 

Mapema Balozi wa Tanzania Mjini Washington D.C Bibi Mwanaidi Sinare Maajar alisema Zanzibar bado ina Utajiri wa Kihistoria ambao Wamarekani walio wengi wanaendelea kuushangaa. 

Balozi Mwanaidi alisema utafiti unaonyesha kwamba soko zuri liliopo la Utalii kati ya Marekani na Tanzania linafaa kutumiwa vyema kwa kuweka mazingira yatakayostawisha pande zote mbili. 

Alisema yapo Makampuni kadhaa ambayo tayari yameshaonyesha nia ya kutaka kuitumia fursa hii ya uwekezaji katika Sekta ya Utalii baada ya kutembelea na kuona maeneo mbali mbali Bara na Hapa Zanzibar. 

Nao kwa upande wao Mabalozi hao wa Heshima wa Tanzania Bwama Ahmed Issa Alqassim wa San Francisco na Bwana Kjell Berg wa Minessota wameahidi kutekeleza vyema majukumu yao waliokabidhiwa na Taifa. 

Mabalozi hao wameishauri Serikali na Jamii kuhakikisha ule Utalii wa Kiutamaduni { Culture Tourism } ulioanzishwa na Vizazi vilivyopita unafaa kulindwa na kuenziwa. Walisema Utalii huu ambao zaidi umejikita katika eneo la Kivazi cha asili umekuwa maarufu na kufikia hatua ya kuigwa na watu maarufu katika sehemu mbali mbali Duniani. 

Wakati wa usiku Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alijumuika pamoja na Wafanyabiashara Waandamizi waliounda kundi la VIP Safari kutoka Nchini Marekani katika chakula cha Usiku. 

Tafrija hiyo iliyoshirikisha pia Baadhi ya Mawaziri pamoja na Watendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar ilifanyika katika Hoteli ya Serena Inn iliyopo Shangani Mjini Zanzibar. 

Akizungumza na Wafanyabiashara hao Balozi Seif alisisitiza kwamba mchango wa Wafanyabiashara hao unaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa sekta binafsi katika uimarishaji wa Uchumi wa Zanzibar. 

Balozi Seif alisema Serikali hivi sasa imelenga kuimarisha Sekta hiyo kwa kuongeza miundo mbinu itakayowezesha kundi kubwa la Vijana wasio kuwa na kipato kupata ajira.

 Mapema akitoa shukrani zake Waziri wa Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema Marekani hivi sasa imekuwa Mshirika mkubwa wa Zanzibar katika Masuala ya Biashara na Uwekezaji. 

Hivyo aliwaomba Wafanyabiashara hao kupitia ofisi za Kibalozi za Tanzania zilizomo ndani ya Majimbo tofauti ya Nchi hiyo kuendelea kuitangaza Zanzibar kwa Wawekezaji wa Majimbo yao.
Na
  Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment