Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na
Mabalozi wa Heshima wa Tanzania katika baadhi ya Majimbo ya Marekani
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Kulia yake ni Balozi wa Tanzania Washington D.C Bibi Mwanaidi Sinare,
Bwana Kjell Berg Minessota na Bwana Ahmed Issa Alqassim San Francisco.
Kushoto ya Balozi ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Dr. Khalid Slum Moh’d, Naibu wake Nd. Said Shaaban pamoja na
Bwana Saleh ambae ni Msaidi wa Balozi Jimbo la Washington.
Makamu wa Pili wa Rais wa Znzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa zawadi kwa
mmoja wa Wafanyabiashara Waandamizi waliounda Kundi la VIP Safari
kutoka Nchini Marekani ambao wapo Nchini kuangalia uwezekano wa namna ya
Kampuni zao kuwekeza Vitega Uchumi Nchini Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Alio Iddi akiwa katika
picha ya pamoja na Ujumbe wa wa Wafanyabiashara waandamizi wa Kundi la
VIP Safari baada ya kuwaandalia chakula cha usiku hapo Serena Inn Hoteli
Shangani Mjini Zanzibar.
Kulia ya Balozi Seif ni Balozi wa Tanzania Washington D.C Bibi Mwanaidi
Sinare na Balozi wa Heshima MjiniMinessota Bw. Kjell Berg.
Kushoto yake ni Waziri wa Hbari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said
Ali Mbarouk, Mke wa Balozi Seif Mama Asha Suleimana Iddi pamoja na Mmoja
wa Wafanyabiashara hao wa VIP Safari.Picha na Saleh Masoud
---
Na Othman Khamis Ame
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema
Mazingira ya Kimaumbile yaliyoizunguuka Zanzibar bado yana fursa nzuri
ya kutumiwa katika shughuli za Uwekezaji Vitega Uchumi.
Balozi Seif alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Mabalozi wawili wa
Heshima wa Tanzania katika majimbo mawili ya Marekani ya Minessota na
San Francisco hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mabalozi hao Bwana Ahmed Issa Qassim atakayeiwakilisha Tanzania katika
Jimbo la San Francisco na Bwana Kjell Berg wa Jimbo la Minessota
waliongozwa na Balozi wa Tanzania Mjini Washington D.C Balozi Mwanaidi
Sinare Maajar.
Balozi Seif alisema katika kuyatumia vyema mazingira hayo Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inajaribu kuongeza nguvu za uimarishaji wa miundo
mbinu katika Sekta ya Utalii.
Alisema licha ya Sekta ya kilimo kuchukuwa nafasi kubwa ya Uchumi wa
Taifa lakini eneo la utalii pia lina fursa nzuri ya kuwa muhimili wa
Pili wa Uchumi wa Zanzibar kwa hivi sasa.
Balozi Seif alifahamisha kwamba serikali inaangalia pia uwekezaji wa
maeneo ya Kumbi za Mikutano ya Kiutalii kutokana na kupanuka zaidi kwa
sekta hiyo hivi sasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaomba Mabalozi hao wa
Heshima wa Tanzania katika Majimbo ya Marekani kuwa wawakilishi wazuri
wa kuitangaza Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kwa wawekezaji kwenye
majimbo watakayoyafanyia kazi.
Balozi Serif aliwaahidi wawakilishi hao kwamba Serikali zote mbili
zitajitahidi kutoa msaada kwao kwa vile kazi watakazokwenda kuzifanya ni
kwa ajili ya Watanzania.
Mapema Balozi wa Tanzania Mjini Washington D.C Bibi Mwanaidi Sinare
Maajar alisema Zanzibar bado ina Utajiri wa Kihistoria ambao Wamarekani
walio wengi wanaendelea kuushangaa.
Balozi Mwanaidi alisema utafiti unaonyesha kwamba soko zuri liliopo la
Utalii kati ya Marekani na Tanzania linafaa kutumiwa vyema kwa kuweka
mazingira yatakayostawisha pande zote mbili.
Alisema yapo Makampuni kadhaa ambayo tayari yameshaonyesha nia ya kutaka
kuitumia fursa hii ya uwekezaji katika Sekta ya Utalii baada ya
kutembelea na kuona maeneo mbali mbali Bara na Hapa Zanzibar.
Nao kwa upande wao Mabalozi hao wa Heshima wa Tanzania Bwama Ahmed Issa
Alqassim wa San Francisco na Bwana Kjell Berg wa Minessota wameahidi
kutekeleza vyema majukumu yao waliokabidhiwa na Taifa.
Mabalozi hao wameishauri Serikali na Jamii kuhakikisha ule Utalii wa
Kiutamaduni { Culture Tourism } ulioanzishwa na Vizazi vilivyopita
unafaa kulindwa na kuenziwa.
Walisema Utalii huu ambao zaidi umejikita katika eneo la Kivazi cha
asili umekuwa maarufu na kufikia hatua ya kuigwa na watu maarufu katika
sehemu mbali mbali Duniani.
Wakati wa usiku Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alijumuika pamoja na Wafanyabiashara Waandamizi waliounda kundi la VIP
Safari kutoka Nchini Marekani katika chakula cha Usiku.
Tafrija hiyo iliyoshirikisha pia Baadhi ya Mawaziri pamoja na Watendaji
wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar ilifanyika katika Hoteli ya Serena Inn
iliyopo Shangani Mjini Zanzibar.
Akizungumza na Wafanyabiashara hao Balozi Seif alisisitiza kwamba
mchango wa Wafanyabiashara hao unaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa
sekta binafsi katika uimarishaji wa Uchumi wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Serikali hivi sasa imelenga kuimarisha Sekta hiyo
kwa kuongeza miundo mbinu itakayowezesha kundi kubwa la Vijana wasio
kuwa na kipato kupata ajira.
Mapema akitoa shukrani zake Waziri wa Habari, Utamaduni,Utalii na
Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema Marekani hivi sasa imekuwa Mshirika
mkubwa wa Zanzibar katika Masuala ya Biashara na Uwekezaji.
Hivyo aliwaomba Wafanyabiashara hao kupitia ofisi za Kibalozi za
Tanzania zilizomo ndani ya Majimbo tofauti ya Nchi hiyo kuendelea
kuitangaza Zanzibar kwa Wawekezaji wa Majimbo yao.
Na
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment