Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, July 11, 2012

CLOUDS 'WAUZIWA' SIMBA NA AZAM, SASA KUPIGWA ALHAMISI DAR




MUINGEREZA; Stewart Hall wa Azam
MECHI ya fainali ya Kombe la Urafiki kati ya Azam na Simba sasa itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Alhamisi na itasimamiwa na kampuni ya Prime Time Promotions, wamiliki wa Clouds Media Group.
Msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba mazungumzo yanaendelea kuhusu mustakabali wa mechi hiyo, lakini kwa sasa jukumu la promosheni ya mechi wamekabidhiwa Prime Time.
Munir amesema sababu za mechi hiyo kuhamishiwa Dar es Salaam ni kwamba Simba na Azam zimeukataa Uwanja wa Amaan kwamba ni mbovu na wachezaji wake wanaumia.
Mapema leo, kocha wa Azam FC, Stewart Hall kutoka Uingereza alisema ana matumaini ya kuwafunga Simba SC kwenye fainaili, wakati mpinzani wake Mserbia Profesa Milovan Cirkovick alimjibu kwamba anajidanganya.
Stewart amesema mjini hapa, baada ya ushindi wa 2-0 jana dhidi ya mabingwa wa Zanzibar, Super Falcon na kutinga fainali, sasa ni zamu ya mabingwa wa upande wa pili wa Muungano, Simba SC nao kula kichapo.
Lakini Stewart amekiri kwamba Simba, mabingwa wa Bara ni timu nzuri na mchezo utakuwa wa ushindani, lakini mwisho wa siku, Azam watang’ara.
Stewart amesema wachezaji wake aliowapa mapumziko kama Mrisho Khalfan Ngassa na John Raphael Bocco ‘Adebayor’ wataendelea kuwa watazamaji, kwani ataendelea na kikosi kile kile kilichomfikisha hapa.
Kwa upande wake, Milovan amesema tangu wanapanda boti kwenda Zanzibar alijua tu fainali itakuwa kati ya timu yake na Azam kwa sababu hizo kwa sasa ndizo timu bora Tanzania.
“Sisi mabingwa, wao wa pili kwenye Ligi, hao ndio wapinzani wetu. Hatuwezi kuukwepa ukweli huo. Ila wataendelea kuwa wa pili hata baada ya dakika 90,”alisema Milovan.
Milo alisema amewaona Azam wakicheza Zanzibar na anakiri ni timu nzuri, lakini ya kiwango cha kuisumbua tu Simba SC si kuizuia kushinda.
Azam walikuwa wa kwanza jana kujikatia tiketi ya kuingia fainali, baada ya kuifunga Falcon 2-0, mabao yote yakitiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Herman Tcheche Uwanja huo huo wa Amaan, Zanzibar.
MSERBIA; Profesa Milovan Cirkovick wa Simba SC
Tcheche alifunga bao la kwanza dakika ya 67, akiunganisha krosi ya Hamisi Mcha wakati bao la pili, alifunga kwa penalti, dakika ya 77, baada ya Samir Haji Nuhu kuangushwa kwenye eneo kla hatari na Samir Said dakika ya 77.
Katika mechi hiyo, Azam ilipata pigo dakika ya 54, baada ya mshambuliaji wake Gaudence Exavery Mwakimba kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 54 kwa kumpiga kiwiko Abdul Ally.
Simba nayo ilijikatia tiketi yake baadaye hiyo jana kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Zanzibar All Stars, bao pekee la kiungo wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Patrick Kanu Mbivayanga.
Kanu, aliyeletwa kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu na Mkongo mwenzake, marehemu Patrick Muteesa Mafisango, alifunga bao hilo dakika ya 57, akiunganisha krosi ya mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr., aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Salim Kinje.
Dakika ya 85, Sabri Ramadhan ‘China’wa All Stars, alikwamisha mpira nyavuni, lakini refa akasema alikuwa ameotea.. na bin zubeiry

No comments:

Post a Comment