Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, July 11, 2012

NCCR yafikiria kumsamehe Kafulila



MGOGORO baina ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na Uongozi wa chama chake cha NCCR-Mageuzi, umeelekea kupata suluhu baada ya chama hicho sasa kuamua kumsamehe.

Mvutano huo uliosababisha mbunge huyo kijana kuvuliwa wadhifa wa Ukatibu Mwenezi na baadaye yeye na wenzake watano kuvuliwa uanachama, uliibuka mwishoni mwa mwaka jana baada ya kudaiwa kuzungumza mambo ya ndani ya chama katika vyombo vya habari.

Kufuatia uamuzi huo Kafulila alifungua kesi Mahakama Kuu  kupinga uamuzi huo, ambapo mahakama ilitoa agizo la kusitisha maamuzi hayo mpaka kesi hiyo ya msingi itakapomalizika, hivyo kumfanya Kafulila kuendelea kuwa mbunge.



Taarifa zilizolifikia Gazeti hili jana zinaeleza kuwa pande hizo mbili zimeona ni muhimu kuafikiana na kurudi katika meza ya mazungumzo nje ya mahakama ili kukiimarisha chama hicho.

Zilieleza kuwa suala hilo ni moja ya ajenda zilizojadiliwa katika kikao cha Halmashauri Kuu  kilichofanyika wiki moja na nusu iliyopita baada ya kuibuliwa na mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu mkuu wa chama hicho, Samwel Ruhuza alisema Kafulila ameomba msamaha na kusisitiza kuwa hivi sasa amebadilika huku akipinga vikali kuwa suala hilo lilijadiliwa katika kikao hicho.


“Suala hili halikujadiliwa kabisa katika Nec iliyoketi hivi karibuni, ndio maana haikuwa ajenda  kubwa,” alisema Ruhuza.

Licha ya kutokuwa tayari kueleza msamaha huo uliombwa kwa maandishi au kwa maneno, Ruhuza alisema, “Msamaha ni msamaha na jambo hili nisingependa kulieleza kiundani zaidi kwa kuwa litaamuliwa na vikao vya chama, pia limeshafika mahakamani.”

No comments:

Post a Comment