- MWANDISHI WA BBC AMSHUHUDIA AKIPUMULIA MASHINE KATIKA HOSPITALI MOJA AFRIKA KUSINI, MKUU WA JOPO LA MADAKTARI
AFYA
ya Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka
aliyeanza matibabu akiwa chini ya uangalizi maalumu wa madaktari (ICU),
baada ya kutekwa, kupigwa na kisha kutupwa kwenye pori la Pande nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ni mbaya, Mwananchi limeelezwa.Habari
zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa daktari huyo wa magonjwa
ya binadamu, sasa hajitambui na anapumulia mashine katika moja ya
hospitali za nchini Afrika Kusini alikolazwa kwa matibabu hayo.
Dk
Ulimboka ambaye awali kulizuka utata wa mahali alipo; Afrika Kusini au
Ujerumani, sasa imethibitika kuwa yuko Afrika Kusini, lakini hali yake
ni mbaya.
"Ukweli ni kwamba yuko Afrika Kusini, lakini taarifa tulizozipata leo
(jana) asubuhi ni kwamba sasa amelazwa ICU akiwa hajitambui kabisa,"
alisema mmoja wa madaktari wanaofuatilia kwa karibu matibabu ya
Ulimboka.
Aliendelea, "Sasa hajitambui na tumwombe Mungu tu afanye miujiza yake."
Kiongozi wa Jopo la Madaktari linaloshughulikia matibabu ya Dk Ulinboka,
Profesa Joseph Kahama alisema amezisikia taarifa hizo zikitangazwa na
Kituo cha Utangazaji cha Uingereza, (BBC) jana asubuhi, lakini hajaweza
kuzithibitisha.
"Asubuhi wote tulisikia kwamba hali yake (Dk Ulimboka) ni mbaya na yuko
kwenye 'koma', lakini taarifa hizo sijazithibitisha kujua zina ukweli
kiasi gani," alisema.
Mwananchi liliwasiliana na mwandishi wa BBC Afrika Kusini, Omary Mutasa
ambaye alisema kwamba, ni kweli alikwenda kwenye hospitali (jina
linahifadhiwa kwa sasa) alikolazwa Dk Ulimboka ambako alimkuta akipumua
kwa usaidizi wa mashine na alikuwa hawezi kuongea.
“Niliingia hadi sehemu alikolazwa Dk Ulimboka, nimeona akipumua kwa
usaidizi wa mashine, hata ndugu zake walishtuka sana kuniona pale na
hawakufurahishwa mimi kwenda pale,” alisema katika mahojiano ya simu na
Mwananchi.
Mutasa alisema kwamba, jana jioni alikwenda hospitali kuangalia hali yake inaendeleaje, lakini hakuweza kumwona.
“Nimejaribu kwenda tena jioni kupata taarifa za hali yake, lakini
nimeshindwa kumwona. Utawala wa hospitali ulinikatalia kabisa,”
alisema.
Jana asubuhi, Mutasa aliripoti katika kipindi cha asubuhi cha BBC kwamba
hali ya Dk Ulimboka ni mbaya na kalazwa katika chumba cha wagonjwa
mahututi na anapumulia mashine.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Madaktari (MAT), Dk Rodrick
Kabangila alisema haelewi uvumi huo umetoka wapi kwani yeye hana taarifa
hizo.
“Mimi bado nashindwa kuelewa kwani nimezungumza na na wenzangu ambao
wanawasiliana na ndugu wa Dk Ulimboka kwa karibu wakasema hakuna
taarifa zozote zile mbaya,” alisema Dk Kabangila.
Naye Rais wa Chama hicho, Dk Namala Mkopi alisema hajawasiliana na Dk
Ulimboka tangu juzi. “Bado sijawasiliana na Dk Ulimboka na hatujapata
taarifa zozote za hali yake kama ni mbaya au vipi,” alisema Dk Mkopi.
Mbowe ataka uchunguzi
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe, ameitaka Serikali kuifanyia kazi Sheria ya Uchunguzi wa vifo
vyenye utata kama ilivyoahidiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika
kikao cha bajeti mwaka jana.
Akizungumza katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu, Mbowe
alisema kutotimizwa kwa ahadi hiyo kunaleta hisia kwamba Serikali
inahusika katika baadhi ya vifo hivyo.
Mbowe alisema kuwapo kwa vifo vya aina hiyo nchini huku baadhi yake
vikihusishwa na vyombo vya dola, kunahitaji uchunguzi wa kina na
yakinifu utakaofanywa na chombo huru ili kubaini wahusika na kisha
kuwachukulia hatua za kisheria.
“Katika hotuba yako Waziri Mkuu ulikiri kuwepo kwa tatizo hilo na
ulisema sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata itafanyiwa kazi na
vifo vyenye utata vitafanyiwa uchunguzi, pengine unaweza kutwambia ni
upi utekelezaji wa ahadi yao hiyo?” alisema Mbowe wakati anamwuliza
swali Waziri Mkuu.
Mbowe alisema hisia za dola kuhusika katika mauaji na mateso haya ya
raia zimekuwa zikikuwa kila kukicha na hivyo taifa limepata sifa mbaya
katika anga za kimataifa hasa baada ya kipigo cha Kiongozi wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk Stephen Ulimboka na wabunge wa Chadema jijini Mwanza.
Akijibu swali hilo Waziri Pinda alisema si kweli kuwa taifa linapata sifa mbaya kutokana na tukio la kupigwa kwa Dk Ulimboka.
“Sikubaliani na hoja kuwa sifa ya nchi imeharibika. Kwa lipi? Ukisema
hivyo uwe na ushahidi wa hilo. Vilevile ukitumia mfano wa Ulimboka si
mzuri. Jambo hili linahitaji kupatikana ukweli kwanza. Sasa tumeagiza
uchunguzi wa kina na wa haraka kufanyike ili tupate ukweli huo,” alisema
Pinda.
Kuhusu sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata, Waziri Mkuu Pinda
alisema ni kweli aliahidi kwamba sheria inahitaji kufanyiwa marekebisho
na kwamba tayari vyombo husika vimepewa maelezo ili kuwezesha mabadiliko
hayo kufanyika.
“Wakati mwingine ni uzembe na ufuatiliaji duni. Si kweli kuwa Serikali
inahusika. Sisi (Serikali) tutaendelea kufuatilia jambo hilo kwa umakini
na kuhakikisha sheria hiyo inaanza kufanya kazi,” alisema Pinda.
Habari na Ibrahim Yamola, Fredy Azzah, Florence Majani, Dodoma
Chanzo - http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment