Pages

Friday, July 27, 2012

HAKIMU ATOKA NJE YA MAHAKAMA NA KUZICHAPA KAVU KAVU NA MWANANCHI.

Habari na Ezekiel Kamanga,Iyula Mbozi.
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo,Kata ya Iyula,Tarafa ya Iyula,Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya Mheshimiwa Grace Kivelege aliuacha Ukumbi wa mahakama hyo na kutoka nje kisha kuanza kuzozana na mwananchi mmoja Bwana Sebastian Kilindu aliyekuwa amefika mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi.

Sababu ya ugomvi huoni pale Hakimu huyo alipomtaka mshitakiwa Bwana Laurence Julias,kuingia mahabusu ndipo Bwana Kilindu alipinga hali iliyompelekea hakimu kumkunja shingoni na kuamuliwa na mwandishi wa habari hizi,huku wananchi wakishangilia zogo hilo wakitaka Hakimu apigwe kutokana na kinachodaiwa kuwa kajijengea mazingira ya rushwa.

Baada ya kuamuliwa hakimu huyo alimfuata tena Bwana Kilindu na kumkunja mbele ya Kituo cha Polisi cha Iyula,Wilayani Mbozi huku akiporomosha matusi ya nguoni na kushangaza wananchi baada ya kuzivunja sheria ili hali kapewa dhamana ya kuzisimamia.

Aidha,kesi hiyo iliyokuwa ikimhusisha Bwana Laurence ambaye amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu na baadae kukata rufaa katika Mahakama ya wilaya ya Mbozi na kuachiwa huru lakini alibambikiziwa kesi nyingine akidaiwa kuwapiga wananchi watatu wanaoishia katika Kijiji cha Ichesa wilayani humo.

Mtuhumiwa Laurence amekuwepo jela kwa muda wa mwezi mmoja,ambapo ndugu na jamaa walifika siku ya Jumatatu Julai 23 mwaka huu kwa ajili ya kuomba kumwekea dhamana ambapo Hakimu huyo Bi.Kivelege alikataa na kuwataka wafike siku inayofuata Julai 24 wakiwa na barua ya udhamini.

Aidha,walipofika siku hiyo Julai 24 mwaka huu wakiwa na barua ya udhamini,bado hakuwasikiliza hadi ilipofika majira ya saa 9:30 alasiri ndipo alipotoa hati ya kumtoa gerezani na mshitakiwa kufikishwa Kituo cha Polisi cha Iyula majira ya saa 12:30 jioni na kudhaminiwa na kaka yake mbele ya Mkuu wa kituo hicho Mkaguzi msaidizi Inspekta Uziweli Mwanga ambapo alitakiwa kufika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi inayomkabili.

Julai 25 mwaka huu mshitakiwa alifika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi inayomkabili lakini kabla ya kesi Bwana Laurence Julias aliwasilisha barua yenye sababu ya kumpinga hakimu huyo,ambapo sababu ya kwanza akidai hana imani naye, ya pili yupo karibu na walalamikaji na mwisho alidai kwamba kesi yake aliomba kutosikilizwa na hakimu huyo ambaye alitoa hukumu ya kwenda jela miaka mitatu bila sababu ya msingi.

Kufuatia hali hiyo Hakimu Bi Kivelege alionekana kukasirishwa na barua hiyo,hivyo kumtaka mshitakiwa adhaminiwe upya na kumamuru Mkuu wa Kituo cha polisi kumweka mahabusu hali iliyowakasirisha ndugu zake na kuleta tafrani kubwa katika kituo hicho.

Hata hivyo baada ya kuona hali hiyo Mkuu wa kituo hicho cha Polisi Inspekta Mwanga alimrejesha Bwana Laurence mahakamani ndipo zogo lililopoanza,hakimu akitaka dhamana ya awali ifutwe huku sababu za kufutwa hazikuwekwa bayana.

Wakati huohuo Hakimu hakuendelea na kesi huku akiondoka na gari yake akiacha kesi nyingine bila kusikilizwa lakini katika uchunguzi uliofanya ulibaini kuwa jumla ya kesi 9 zilizohukumiwa na hakimu huyo zimekatiwa rufaa kutokana na watuhumiwa kuachiwa huru mahakama ya wilaya hali inayotia shaka utendaji kazi wake.
                                        SOURCE http://chimbukoletu.blogspot.com

No comments:

Post a Comment