Saed
Kubenea - Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi inayochapisha
gazeti la Mwana Halisi akionesha baadhi ya Magazeti yaliyolalamikiwa na
Serikali
WAKATI
Mkurugenzi Mtendaji wa Gazeti la MwanaHalisi, Saed Kubenea akiitaka
Serikali kuondoa amri ya kulifungia gazeti lake, Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF) limetoa tamko juu ya suala hilo.
Kubenea
aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Sheria ya Magazeti ya
mwaka 1976 ni katili kwa sababu haishauri Serikali kutoa maelezo ama
kukumweleza mwenye gazeti juu ya nia ya kulifunga.
Kubenea
alilazimika kuwaeleza waandishi juu ya suala hilo kufuatia kitendo cha
Serikali kulifungia Gazeti la MwanaHalisi kwa kile ilichodai kuwa
mwenendo wake wa kuandika habari na makala ni wa kichochezi, uhasama na
uzushi.
Alisema
yeye hakuitwa kujitetea , bali alipata barua kutoka Maelezo iliyokuwa
na maelekezo ya kwamba amezuiwa kutoa gazeti na kwamba asome kwenye
gazeti la Serikali namba 258 la Julai 27, mwaka huu. “Sheria hii katili
ya magazeti ingali hai. Haijafutwa. Watawala wanaihitaji. Wanaitumia
kutunyang’anya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na kuwasiliana,
wamefanya hivyo kwa Mwanahalisi. Wametishia kufanya hivyo kwa vyombo
vingine vya habari. Hii ni hatari,”alisema Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Licha
ya kuitaka Serikali kuondoa amri ya kulifungia gazeti lake, Kubenea
pia aliwaomba wasomaji wao na wadau wengine wa habari kusimama nao
katika kudai huru na haki ya kutafuta na kusambaza habari kwa sababu
nchi hii ni yetu sote.
Katika
hatua nyingine, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limelaani kitendo
cha kufungiwa kwa Gazeti la Mwanahalisi, likitoa maelezo kuwa lengo la
Serikali ni kuviziba midomo vyombo vya habari ili visifichue uovu
unaofanywa katika mfumo wa utawala.
Taarifa
ya jukwaa hilo ilisema kuwa, sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo
Serikali imeitumia kulifungia gazeti hilo, ni moja ya sheria ambazo
zimekuwa zikilalamikiwa na kuwa mara kadhaa yamekuwapo mapendekezo
kwamba sheria hizo zifutwe.
“Uamuzi
wa kulifungia MwanaHalisi haukubaliki na tunauona kama mwendelezo wa
jitihada za Serikali kukandamiza uhuru wa habari na wanahabari nchini,
lengo likiwa ni kuwaziba midomo wasiseme ukweli kuhusu uovu unaofanyika
katika mfumo wetu wa utawala na jamii kwa ujumla,” ilisema sehemu ya
taaifa ya TEF iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake, Neville Meena.
Ilisema
pia kuwa, uamuzi huu wa Serikali unaonekana una nia mbaya ndani yake,
kwani adhabu ya kulifungia kwa muda usiojulikana ina tafsiri pana kwani
inawezekana lengo la Serikali ni kulifuta gazeti la MwanaHalisi kijanja.
Naye
wakili wa gazeti hilo, Legemeleza Nshala alisema Serikali ilikiuka
ibara ya 18 kifungu cha 26 (1) na cha (2) na kifungu cha 30 (1) na cha 8
(2) (a)-(e) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977. Alisema
pia kuwa imekiuka Ibara ya 19 ya Agano la Kimataifa la Haki za
Binadamu la mwaka 1966 na Ibara ya 6 ya Agano la Fungamano la Afrika
Mashariki pamoja na Ibara ya 8 ya Agano la Haki za Binadamu na watu la
Afrika la mwaka 1981.
No comments:
Post a Comment