Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, August 1, 2012

Kubenea, Jukwaa La Wahariri Watoa Tamko Kuhusu MwanaHalisi Kufungiwa



Saed Kubenea - Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi inayochapisha gazeti la Mwana Halisi akionesha baadhi ya Magazeti yaliyolalamikiwa na Serikali

WAKATI Mkurugenzi Mtendaji wa Gazeti la MwanaHalisi, Saed Kubenea akiitaka Serikali kuondoa amri ya kulifungia gazeti lake, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa tamko juu ya suala hilo.

Kubenea aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ni katili kwa sababu haishauri Serikali kutoa maelezo ama kukumweleza mwenye gazeti juu ya nia ya kulifunga.
Kubenea alilazimika kuwaeleza waandishi juu ya suala hilo kufuatia kitendo cha Serikali kulifungia Gazeti la MwanaHalisi kwa kile ilichodai kuwa mwenendo wake wa kuandika habari na makala ni wa kichochezi, uhasama na uzushi.

Alisema yeye hakuitwa kujitetea , bali alipata barua kutoka Maelezo iliyokuwa na maelekezo ya kwamba amezuiwa kutoa gazeti na kwamba asome kwenye gazeti la Serikali namba 258 la Julai 27, mwaka huu. “Sheria hii katili ya magazeti ingali hai. Haijafutwa. Watawala wanaihitaji. Wanaitumia kutunyang’anya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na kuwasiliana, wamefanya hivyo kwa Mwanahalisi. Wametishia kufanya hivyo kwa vyombo vingine vya habari. Hii ni hatari,”alisema Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Licha ya kuitaka Serikali kuondoa amri ya kulifungia gazeti lake, Kubenea pia aliwaomba wasomaji wao na wadau wengine wa habari kusimama nao katika kudai huru na haki ya kutafuta na kusambaza habari kwa sababu nchi hii ni yetu sote.

Katika hatua nyingine, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limelaani kitendo cha kufungiwa kwa Gazeti la Mwanahalisi, likitoa maelezo kuwa lengo la Serikali ni kuviziba midomo vyombo vya habari ili visifichue uovu unaofanywa katika mfumo wa utawala.

Taarifa ya jukwaa hilo ilisema kuwa, sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo Serikali imeitumia kulifungia gazeti hilo, ni moja ya sheria ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na kuwa mara kadhaa yamekuwapo mapendekezo kwamba sheria hizo zifutwe.

“Uamuzi wa kulifungia MwanaHalisi haukubaliki na tunauona kama mwendelezo wa jitihada za Serikali kukandamiza uhuru wa habari na wanahabari nchini, lengo likiwa ni kuwaziba midomo wasiseme ukweli kuhusu uovu unaofanyika katika mfumo wetu wa utawala na jamii kwa ujumla,” ilisema sehemu ya taaifa ya TEF iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake, Neville Meena.

Ilisema pia kuwa, uamuzi huu wa Serikali unaonekana una nia mbaya ndani yake, kwani adhabu ya kulifungia kwa muda usiojulikana ina tafsiri pana kwani inawezekana lengo la Serikali ni kulifuta gazeti la MwanaHalisi kijanja.

Naye wakili wa gazeti hilo, Legemeleza Nshala alisema Serikali ilikiuka ibara ya 18 kifungu cha 26 (1) na cha (2) na kifungu cha 30 (1) na cha 8 (2) (a)-(e) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977. Alisema pia kuwa imekiuka Ibara ya 19 ya Agano la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1966 na Ibara ya 6 ya Agano la Fungamano la Afrika Mashariki pamoja na Ibara ya 8 ya Agano la Haki za Binadamu na watu la Afrika la mwaka 1981.



No comments:

Post a Comment