Jeshi la Polisi Mkoani Tabora kwa kushirikiana
na raia wema wamefanikiwa kuwakamata watu watatu wanaotuhumiwa kuhusika na Mauaji
ya Watu wawili ambao ni Mke na Mume tarehe 09 Julai mwaka huu katika Kijiji cha
Inala Kata ya Ndevelwa Manispaa ya Tabora.
Watu hao wanatuhumiwa kuwaua kwa kuwakatakata
na panga Khalid Said (55) na Amina Ally (50) usiku wa siku hiyo wakati
walipokuwa wamepumzika nje ya nyumba yao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kamanda
wa Polisi Mkoani Tabora Kamishna Msaidizi wa Polisi Anthony Rutta aliwataja
watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa ni Mheshimiwa Shakalambe (55) Mkazi wa Naila,
Jumanne Mohamed (30) Msukuma mkazi wa Mbalala Kigwa na Mabula Masanja (33)
Msukuma Mkazi wa Mbuyuni Kigwa.
Kamanda Rutta alisema watu hao walikamatwa
katika msako mkali uliofanywa na Jeshi hilo
mkoani humo ambapo pia wamekutwa na Panga ambalo walilitumia katika kutekeleza
mauaji hayo.
“Watu hawa walitumia mbinu ya kujifanya kuwa
ni wanunuzi wa Ngo’mbe lakini wakati wakiendelea kujadili biashara hiyo
walitokea Vijana wawili ambao kila mmoja wao alikuwa na Panga pamoja na fimbo
ndipo wakatekeleza unyama huo na wamedai kuwa waliahidiwa kulipwa milioni moja
au Ngo’mbe wawili kwa kazi hiyo”
Watuhumiwa hao watafikishwa Mahakamani mara
tu baada ya upelelezi kukamilika na Kamanda Rutta ametoa wito kwa Wananchi
kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kukomesha Vitendo vya Mauaji na
kuwafichua Wahalifu wa makosa mbalimbali.SOURCE FULLSHANGWE
No comments:
Post a Comment