WAKATI
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ikitoa kipaumbele kwa kilimo na
kutangaza mpango wa kilimo kwanza, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa
amepingana na dhana hiyo kwa kusema elimu ndiyo inayopaswa kuwa kwanza
na baadaye kilimo.
Lowassa
alitoa wito huo wakati alipokuwa akikabidhi michango ya harambee ya
wafugaji wa jamii ya Wamasai katika Kijiji cha Kiegea kusaidia ujenzi wa
Shule ya Msingi Ujirani ambapo alialikwa kuwa mgeni rasmi kama kiongozi
wa jamii hiyo nchini.
Lowassa
ambaye anatamba kwa kuasisi mpango wa shule za kata, alisema elimu ni
muhimu zaidi kabla ya kilimo, hivyo alitoa changamoto kwa wananchi wa
kata mpya ya Mkundi ya jamii hiyo ya wafugaji kuanza ujenzi wa shule ya
sekondari ya kata.
“'Ni
aibu kata hii kutokuwa na shule ya sekondari wakati kila kata nchini
ina shule ya sekondari ambako hivi sasa angalau kuna usawa kwa watoto
kugusa elimu ya sekondari,” alisema na kuongeza kuwa atakuwa tayari
kurudi kwenye kata hiyo Januari mwakani kuongoza harambee ya kuchangisha
fedha za ujenzi wa sekondari.
“Niko
tayari kuja Januari kuongoza harambee ya kuchangisha fedha, ni aibu,
kwakweli sijafurahishwa na hali yenu hapa, mnatakiwa nyinyi wenyewe
msimame kidete kujiletea maendeleo, njooni Monduli mjifunze jinsi
wafugaji wenzenu walivyoweza kutumia mifugo yao kujenga shule na nyumba
za walimu,” alisema Lowassa.
Katika
hilo, alimtaka kila mfugaji kutoa ng’ombe au mbuzi mmoja kwa ajili
yakuchangia elimu kwenye kata yao na kumuomba mkuu wa wilaya kutumia
sheria zilizopo kumkamata na kumtia ndani yeyote atakayekaidi wito huo.
Katika
harambee hiyo, Lowassa alichangia mabati 500 kwa ajili ya kumalizia
ujenzi wa madarasa ya shule hiyo ya msingi ya Ujirani yenye wanafunzi
414, na walimu wawili tu; mmoja wa kuajiriwa na mwengine wa kujitolea.
Wananchi
wa eneo hilo walichanga ng’ombe watano kwa ajili ya kuendeleza shule
hiyo, idadi ambayo Lowassa aliipinga akisema kuwa wananchi hao wana
idadi kubwa ya mifugo hivyo wanatakiwa watoe zaidi.
Hii ni mara ya pili kwa Lowassa kupingana na serikali katika suala la vipaumbele vya taifa.
Hivi
karibuni Waziri Mkuu huyo mstaafu alishupalia suala la ajira kwa vijana
kwamba ni bomu linalosubiri kulipuka, kauli ambayo ilijibiwa kwa nguvu
na serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
source tanzania daima
No comments:
Post a Comment