Gazeti la habari leo la tarehe 5 Agosti, 2012 liliripoti kwamba, mkazi mmoja wa kijiji cha Mubinyage Ngara mkoani Kagera, Adam Balekawe (32) alidaiwa kufanya mauaji ya kinyama kwa kumchoma sindano ya sumu na kumnywesha sumu mtoto wake mwenye umri wa miezi tatu, Amani Adam, akihofia kuchekwa na ndugu kwa kuzaa na Ombeni Paschal (27) mwanamke mwenye ulemavu.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imesikitishwa na taarifa
ya mauaji ya mtoto huyo mdogo asiyekuwa na hatia. Aidha, Wizara imesikitishwa na sababu za unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu jambo ambalo limepelekea mtoto huyo kuuawa na baba yake kwa kuwa tu mama wa mtoto ni mlemavu.
Wizara inakemea na kulaani vikali mauaji ya mtoto huyo na inapenda kusisitiza kwamba watu wenye ulemavu wanayo haki na nafasi katika jamii sawa na watu wengine. Vilevile jamii itambue kuwa watu wenye ulemavu wanahaki ya kuthaminiwa utu wao na kushiriki haki zote za msingi. Aidha, kitendo kilichofanywa na baba wa mtoto huyo kimechochewa
na mazingira na mitizamo finyu katika jamii kuhusu walemamvu jambo
ambalo linachangia unyanyapaa kwa kundi hili ambao unasababisha kutengwa kwao katika maisha na shughuli za kila siku katika jamii zetu. Wizara inapenda kueleza kuwa mtizamo huo ni hasi na unakwenda kinyume na haki za binadamu hivyo ni budi wananchi kuachana na mila na imani zenye ukatili wa kupokonya haki ya ambayo ndio haki kuu zaidi ya haki zote.
Katika
tukio lingine imeripotiwa kuwa mkazi wa kijiji cha Ndelema Crispin
Lwela (26) anadaiwa kumbaka kisha kufanya mauaji ya kinyama kwa
kumchinja na kisu mtoto wake mwenye umri wa miaka mitatu. Wizara
imesikitishwa na tukio hilo na kwa msingi huu Wizara inapenda kuwakumbusha wananchi kwamba Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kwamba binadamu wote ni
sawa na kwamba wanastahili kupata haki sawa bila kujali rangi, kabila
na dini.
Mwisho Wizara inaendelea
kuhimiza jamii kubadilika na kuhakikisha kuwa familia zinakuwa salama
na mahali penye amani miongoni na wanafamilia bila kusahau kulinda na
kuendeleza haki za watoto wote katika jamii. Vilevile
Wizara inatoa pole kwa mama Ombeni Paschal ambaye amefiwa na mtoto wake
mwenye umri mdogo kutokana na kufanyiwa ukatili na baba yake. Aidha
Wizara inaomba mama wa mtoto na wanafamilia wote kuwa wavumilivu katika
kipindi hiki cha majonzi.
No comments:
Post a Comment