Pages

Tuesday, August 7, 2012

TOKA KAGERA:::::AMUUA MTOTO WAKE KWA KUMNYWESHA SUMU,WIZARA YALAANIMAUAJI YA MTOTO AMANI ADAM (WIKI 3) YALIYOTOKEA WILAYA YA NGARA, KAGERA


Gazeti la habari leo la tarehe 5 Agosti, 2012 liliripoti kwamba, mkazi mmoja wa kijiji cha Mubinyage Ngara mkoani Kagera, Adam Balekawe (32) alidaiwa kufanya mauaji ya kinyama kwa kumchoma sindano ya sumu na kumnywesha sumu mtoto wake mwenye umri wa miezi tatu, Amani Adam, akihofia kuchekwa na ndugu  kwa kuzaa na Ombeni Paschal (27) mwanamke mwenye ulemavu.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imesikitishwa na taarifa ya mauaji ya mtoto huyo mdogo asiyekuwa na hatia. Aidha, Wizarimesikitishwa na sababu za unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu jambo ambalo limepelekea mtoto huyo kuuawa na baba yake kwa kuwa tu mama wa mtoto ni mlemavu.
Wizara inakemea na kulaani vikali mauaji ya mtoto huyo na inapenda kusisitiza kwamba watu wenye ulemavu wanayo haki na nafasi katika jamii sawa na watu wengine. Vilevile jamii itambue kuwa watu wenye ulemavu wanahaki ya kuthaminiwa utu wao na kushiriki haki zote za msingi. Aidha, kitendo kilichofanywa na baba wa mtoto huyo kimechochewa na mazingira na mitizamo finyu katika jamii kuhusu walemamvu jambo ambalo linachangia unyanyapaa kwa kundi hili ambao unasababisha kutengwa kwao katika maisha na shughuli za kila siku katika jamii zetu. Wizara inapenda kueleza kuwa mtizamo huo ni hasi na unakwenda kinyume na haki za binadamu hivyo ni budi wananchi kuachana na mila na imani zenye ukatili wa kupokonya haki ya ambayo ndio haki kuu zaidi ya haki zote.
Katika tukio lingine imeripotiwa kuwa mkazi wa kijiji cha Ndelema Crispin Lwela (26) anadaiwa kumbaka kisha kufanya mauaji ya kinyama kwa kumchinja na kisu mtoto wake mwenye umri wa miaka mitatu. Wizara imesikitishwa na tukio hilo na  kwa msingi huu Wizara inapenda kuwakumbusha wananchi kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kwamba binadamu wote ni sawa na kwamba wanastahili kupata haki sawa  bila kujali rangi, kabila na dini.
Mwisho Wizara inaendelea kuhimiza jamii kubadilika na kuhakikisha kuwa familia zinakuwa salama na mahali penye amani miongoni na wanafamilia bila kusahau kulinda na kuendeleza haki za watoto wote katika jamii. Vilevile Wizara inatoa pole kwa mama Ombeni Paschal ambaye amefiwa na mtoto wake mwenye umri mdogo kutokana na kufanyiwa ukatili na baba yake. Aidha Wizara inaomba mama wa mtoto na wanafamilia wote kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha majonzi.

No comments:

Post a Comment