Pages

Monday, August 6, 2012

Wanne Wamekufa Katika Ajali Mlima Kitonga Iringa





Gari ya kampuni ya Asas Iringa ikijaribu kutoa msaada wa kuvuta malori yaliyogongana ili kutoa maiti iliyobanwa na lori.

Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Mohamed Mpinga akiwa katika eneo la tukio.

WATU wanne wamekufa papo hapo na mmoja kujeruhiwa vibaya baada ya malori mawili kugongana na kutumbukia bondeni katika mteremko wa mlima kitonga wilayani Kilolo katika barabara kuu ya Iringa - Dar es Salaam.

Maroli hayo moja lenye shehena kubwa ya madini aina ya shaba na lingine lenye bidhaa mbalimbali za dukani yanalindwa vikali na askari Polisi wa wilaya hiyo, ili kunusuru mali hizo zisiibiwe.

Akizungumza katika eneo la ajali Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Taifa, Mohamed Mpinga alisema kwa masikitiko kwamba ajali nyingi zinazoendelea kutokea nchini zimekuwa zikisababishwa na uzembe wa madereva.

Tarifa kutoka kwa mashuhuda waliokuwepo katika eneo la tukio zimedai kwamba, ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana na kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori lenye namba za usajili T587 BGP aina la Scania.

Mashaka Abdala alisema roli hilo lenye mali mbali mbali za dukani lilikuwa limeharibika na kuegeshwa kando ya barabara hiyo na liligongwa na lori lingine lenye namba za usajili T T319 BDG aina ya Scania pia ambalo breki zake zilikataa wakati likitelemka katika mlima huo.

Akithibitisha vifo vya watu waliokuwemo kwenye maroli hayo, Mpinga alisema taarifa za Polisi zimethibitisha watu wanne kati ya sita waliokuwemo katika maroli hayo kufa hapo huku mmoja akijeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa.

Mbali na majina yao kutofahamika mara moja, mpaka tunakwenda mitamboni maiti moja ilikuwa bado haijatolewa kutoka kwenye kibini ya moja ya maroli hayo kilichopondwa na kufunikwa na kontena za maroli hayo, katika bonde la mlima huo.

Taarifa za kipolisi zimedai kwamba katika ajali hiyo kibini ya roli lilolokuwa limepakia shaba lilifunikwa na kontena za maroli hayo baada ya kwa pamoja maroli hayo kutumbukia katika korongo la mlima huo.

Ajali hiyo ni moja kati ya ajali nyingi zinazoendelea kutokea mkoani Iringa huku ukiwa katika maandalizi ya kitaifa ya kuadhimisha Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.

Kamanda Mpinga aliwakumbusha madereva kuzingatia sheria za barabarani na akahidi kwamba msako mkali wa wale wanaokiuka sheria hizo utaanza kufanywa.

Mpinga alisema kikosi cha usalama barabarani kitaweka utaratibu wa ukaguzi maalumu wa magari katika maeneo ambayo ajali zimekuwa zikitokea mara kwa mara ikiwa ni pamoja na katika mlima huo.
 Chanzo: www.frankleonard.blogspot.com na http://francisgodwin.blogspot.com

No comments:

Post a Comment