Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon (pichani) ametoa
wito kwa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,
kuacha tofauti zao na kumuunga mkono mjumbe wa Umoja wa Mataifa na
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Lakhdar Brahimi, katika juhudi zake za
kuusuluhisha mgogoro wa Syria.
Katika hotuba yake mbele ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Bw.
Ban Ki-Moon amezitahadharisha nchi wanachama kwamba hali nchini Syria
imezorota kupita kiasi.
Amesema ukatili mkubwa na ukiukaji wa haki za binadamu
unaendelea, ukifanywa hasa na upande wa serikali, lakini na upande wa
waasi pia.
Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao
nchini Uingereza, linakadiria kwamba watu wapatao 30,000 wamekwishauawa
nchini humo tangu mgogoro huo ulipoanza takriban miezi 18 iliyopita.
No comments:
Post a Comment