Pages

Monday, September 10, 2012

TAARIFA::::WAANDISHI wa habari nchini kesho wataandamana nchi nzima kwa amani kulaani kuuawa kwa mwandishi mwenzao, Daud Mwangosi aliyeuawa Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Iringa.






NI KESHO ASUBUHI, LENGO NI KULAANI MAUAJI YA DAUD MWANGOSI, KUTOA MATAMKO
Frederick Katulanda
WAANDISHI wa habari nchini kesho wataandamana nchi nzima kwa amani kulaani kuuawa kwa mwandishi mwenzao, Daud Mwangosi aliyeuawa Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Iringa.
Maandamano hayo ambayo yatakuwa ya kimyakimya yatafanyika katika mikoa yote nchini kuanzia saa 2:00 asubuhi na waandishi watakaoshiriki katika maandamano hayo watavaa ama nguo nyeusi au watafunga vitambaa vyeusi mkononi ikiwa ni ishara ya kuomboleza na kulaani kuuawa kwa mwenzao.
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Theophil Makunga alisema kuwa uamuzi wa kufanyika kwa maandamano hayo ulifikiwa katika kikao cha jukwaa hilo kilichofanyika Dar es Salaam juzi.
Alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam, maandamano hayo yamepangwa kuanzia katika Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Mtaa wa Jamhuri ambacho Mwangosi alikuwa akikitumikia na kupita katika Mtaa wa Azikiwe, Barabara ya Bibi Titi hadi katika Viwanja vya Mnazi Mmoja ambako maandamano hayo yatahitimishwa.
Alisema baada ya kufika katika viwanja hivyo, yatapokewa na viongozi wa TEF na kisha baadhi ya waandishi waliokuwapo katika eneo la tukio watatoa ushuhuda wa kilichotokea na kufuatiwa na mjadala kuhusiana na mauaji hayo na kutoa tamko la pamoja.
“Kutatolewa ushuhuda kutoka kwa waandishi wa habari ambao walishuhudia tukio la kuuawa kwa mwandishi mwenzao, wataeleza kwa kina hali halisi na ukweli waliouona siku ya tukio,” alisema Makunga.
Alisema tayari wamekwishawasiliana na Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ambako wamepeleka barua ya kuomba ulinzi kesho wakieleza njia watakazopitia siku hiyo.
“Tunafanya matembezi ya amani, kimyakimya kwa lengo la kulaani tukio la kusikitisha la kuuawa kwa Mwangosi. Ni mwandishi wa kwanza hapa nchini kuuawa akiwa kazini na doa kubwa kwa nchi yetu na vyombo vya dola, hivyo lazima tulilaani tukio hilo.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema, hajapokea barua hiyo na kusema kwamba inawezekana ipo kwa wasaidizi wake na hivyo kuahidi kuifanyia kazi.
“Sijaiona barua yao, inawezekana ipo kwa maofisa wangu au wameipeleka kwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, nitafuatilia kujua ili kuona jeshi langu litafanya nini,” alisema.
Makamu wa Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Jane Mihanji alisema kwamba lengo la maandamano hayo ni kulaani mauaji ya Mwangosi na zaidi ni kufikisha ujumbe kwa Serikali.
“Hatukupendezwa na mauaji hayo, yametuumiza na hatutopenda yatokee tena, tunayalaani na kuomba hatua kali zichukuliwe,” alisema Mihanji.

Maandamano mikoani
Mkurugenzi wa UTPC, Abubakar Karsan alisema, sambamba na maandamano hayo Dar es Salaam, pia waandishi wengine mikoani nao wataandamana kuungana na wenzao kulaani mauaji hayo ya mwenzao.
Maandamano ya mikoa yote nchini yatasimamiwa na klabu zote za waandishi wa mikoa husika na kwamba maandalizi yake ni pamoja na kubainisha njia watakazopitia kwa upande wa mikoani, yamekwisha kamilishwa. Alisema maandamano hayo yatapokewa na wenyeviti wa klabu ambao watatoa matamko mbalimbali kuhusiana na kifo cha Mwangosi.
“Kila mkoa hapa nchini utashiriki maandamano, wataandamana kwa amani kuungana na wenzao kulaani kifo cha mwandishi mwenzao, nao kama ilivyo kwa Dar es Salaam watavaa nguo nyeusi au vitambaa vyeusi mkononi,” alisema.
Alisisitiza kwamba kama itakavyokuwa kwa yale ya Dar es Salaam, maandamano hayo hayatahusisha kiongozi yeyote wa Serikali, chama cha siasa au wanaharakati, bali waandishi wa habari wenyewe viongozi wao.
Mratibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya maandamano hayo yamekamilika. Alisema yataanzia katika Viwanja vya Ghand Hall, kupitia Barabara za Uhuru, Mlango Mmoja, Nyerere na kuingia katika Barabara ya Miti Mirefu, Pamba, Barabara ya Kenyatta hadi Uwanja wa Nyamagana.
Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma, Habel Chidawali alisema, ofisi yake ilikuwa katika maandalizi ya kufanikisha maandamano hayo akisema kwamba hadi leo jioni watakuwa katika nafasi nzuri ya kutangaza njia watakazopitia na mahali yatakapoishia.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya, Christopher Nyenyembe alisema kwamba pia wako katika maandalizi ya kukamilisha maandamano hayo.
“Tunazo sababu za kuandamana kuungana na wenzetu nchi nzima, tulikwisha toa tamko letu kulaani mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kususia kuandika habari za polisi, lakini katika maandamano hayo tutatoa tena tamko,” alisema

No comments:

Post a Comment