JESHI la
Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) pamoja na Jeshi la Kenya
wamethibitisha kupambana na wanamgambo wa al-Shabaab ndani ya mji wa
bandari wa Kismayo, wakidai kukaribia kuuchukua mji huo muhimu
kimkakati.
"Lengo la AMISOM ni kuwakomboa watu wa Kismayo na kuwawezesha kuendelea na maisha yao kwa amani, utulivu na usalama.
Operesheni
zetu zinaendelea kulenga shabaha maalum za al-Shabaab mjini Kismayo,"
alisema Kamanda Andrew Gutti wa AMISOM, akiwataka wapiganaji wote wa
al-Shabaab walio ndani ya Kismayo kuweka chini silaha zao.
Katika
hatua nyengine, Jeshi la Kenya limesema kwamba wapiganaji wake
wamelichukua eneo la kusini ya Kismayo, ngome ya mwisho ya kundi la
al-Shabaab.
Msemaji
wa Jeshi hilo, Cyrus Oguna, aliliambia shirika la habari mapema leo
kwamba wanajeshi wa Kenya walikumbana na upinzani mdogo wakati wa
kuliteka eneo hilo.
WANAJESHI wa Kenya wanaopigana na al-Shabaab nchini Somalia.
Hata
hivyo, wakaazi wa huko pamoja na wanamgambo wa al-Shabaab wamekanusha
taarifa hizo, wakisema kwamba ndio kwanza wanajeshi wa Kenya walikuwa
kwenye viunga vya mbali na Kismayo, ambako wamekuwako kwa zaidi ya siku
nne sasa.
"Maadui
wakitumia mashua za kijeshi walituma mamia ya wanajeshi katika eneo la
pwani jana usiku na mujahidina wetu wanakabiliana nao katika mapigano
makali hivi sasa," alisema kamanda wa al-Shabaab, Sheikh Mohamed Abu
Fatuma, akisisitiza kuwa umbali walipo wanajeshi wa Kenya ni kiasi ya
maili sita kutoka Kismayo.
Wakaadhi
kadhaa pia wa Kismayo walisema kwamba wanajeshi wa Kenya bado walikuwa
ufukweni, walikotia nanga wakiwa kwenye mashua mbili zilizosindikizwa na
helikota za kijeshi, umbali wa kilomita tano kutoka katikati ya mji.
"Mji
wenyewe bado uko chini ya udhibiti wa al-Shabaab. Radio Andalus
inaendelea kufanya kazi, ikiwataka watu kujitokeza kujiunga na jihadi na
kuwafukuza wavamizi," alisema mmoja wa wakaazi hao, Abdulahi Yakub.
Wanajeshi wa Kenya wanaopigana na al-Shabaab nchini Somalia.
MJI wa
bandari wa Kismayo ni ngome kuu ya mwisho mikononi mwa al-Shabaab, ambao
tayari wameshapoteza ngome zao nyengine - ikiwemo miji ya Afgoye,
Baidoa na Marka - kwa kikosi cha wanajeshi 17,000 wa Umoja wa Afrika,
kinachojumuisha pia wanajeshi wa Kenya na Ethiopia.
Jumanne
iliyopita (tarehe 25 Septemba) jeshi la Kenya liliushambulia uwanja wa
ndege wa Kismayo kwa ndege za kijeshi, ikiwa ni sehemu ya operesheni kuu
ya kuingia mji huo.
Tangu
wanajeshi wa Kenya walipoingia nchini Somalia mwaka jana kupambana na
al-Shabaab, wamekuwa wakilenga kuuchukua mji huo. Lakini kufikia lengo
hilo kumewachukua muda mrefu zaidi kuliko walivyokuwa wametarajia.
No comments:
Post a Comment