Pages

Tuesday, October 2, 2012

CUF wapeleka wafuasi Arusha


CUF partylogo.png


CHAMA cha Wananchi (CUF) kimekiri kuwabeba wafuasi wake kutoka jijini Dar es Salaam ili kwenda kuhudhuria mkutano wao uliofanyika jijini Arusha Jumapili iliyopita.
Wafuasi hao waliletwa kwa mabasi kutoka wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke za jijini Dar es Salaam pamoja na maeneo ya Tanga, Arumeru, Singida, Handeni na Moshi.
Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Siasa wa CUF, aliyasema hayo wakati akitoa utambulisho juu ya viongozi waliohudhuria mkutano huo ambapo alisema kuwa wilaya hizo mbali ya kuleta viongozi pia wameleta idadi kubwa ya wanachama.
Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya mabasi ya abiria aina ya Coaster  yaliyowaleta wanachama hao yakiwa yameegeshwa pembeni ya uwanja wa mkutano, yenye namba za usajili T 941 CAK, T 992 BEK, T 393 AXY na T 477 BXA huku yakiwa yamefungwa bendera za chama hicho mbele na nyuma.
Pia kulikuwa na magari aina ya Fuso ambayo hata hivyo namba zake za usajili hazikuweza kufahamika mara moja kutokana na kuzibwa na bendera hizo ambapo mara baada ya mkutano kumalizika, wananchi hao walitangaziwa kuwa warudi kwenye magari yao tayari kwa ajili ya kuanza safari jana asubuhi.
Mkutano huo ulitawaliwa na shamrashamra za hapa na pale baada ya aliyekuwa diwani wa CHADEMA Kata ya Elerai jijini Arusha, John Bayo, aliyefukuzwa na chama chake, kutangaza kujiunga na CUF.
Mbele ya Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wengine, Bayo alisema kuwa yeye aliwahi kuwa mwanachama wa chama hicho mwaka 1992.
Alisema kuwa alishiriki kutafuta wadhamini wa chama hicho kukiwezesha kupata usajili wa kudumu, hivyo ameamua kurudi nyumbani  baada ya kuchoshwa na siasa za fujo.
Alisema kuwa alisikitishwa na uamuzi wa  Kamati Kuu ya CHADEMA yenye wajumbe 45 kumfukuza uanachama bila kuwauliza wananchi wake waliomchagua huku akiendelea kulalamika kuwa hata waasisi wa CHADEMA walijaribu kutafuta suluhu kwa kuwashauri madiwani hao kufuta kesi.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alifika mkutanoni hapo saa 3:46 alasiri akiwa na msafara wa magari ya serikali na ulinzi mkali.
Akizungumza na wananchi, Seif alisema kuwa chama hicho kilisinzia kuweka mizizi mkoani Arusha licha ya kwamba mkoa huo una waasisi wengi wa CUF, hivyo kuahidi kupiga kambi kwa ajili ya kukijenga upya.NA TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment