Denzil L. Doglas, Waziri Mkuu na waziri wa fedha wa Kitt na Nevis’ na ndiye alikuwa akiongoza kikao hicho cha Jumuiya ya Madola.
 Kamalesh Sharma, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.
 
Waziri wa Fedha Mhe.William Mgimwa akibadilishana Mawazo na Mhe. Mwenzake baada ya kikao kizito.
Mawaziri wa Fedha wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola wamekutana leo tarehe 10 oktober hapa jijini Tokyo, kwa madhumuni ya kupitia kazi za jumuiya ya Madola.
“Katika mkutano wetu tulikuwa na agenda kuu nne. Agenda  ya kwanza ilikuwa ni juu ya ukosefu wa ajira kwa vijana; pili,tulizungumzia masuala yote ambayo yalitokana na mikutano iliyopita ambapo suala la ajira lilikuwepo; tatu, tulizungumzia jinsi ya kuhudumia madeni yetu kama nchi wanachama wa Jumuiya ya madola, kwani Jumuiya ya Madola inatoa tahadhari kuhusu madeni ambayo yanaweza yakaiathiri nchi mojawapo kwani kwa kuathirika kwa nchi moja kuna weza kuleta matatizo hata kama nchi nyingine ni tajiri; suala la nne lililozungumziwa katika mkutano huo lilikuwa ni juu ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na nchi zile za kundi la ishirini yaani ( G20)”.alieleza Mhe. Mgimwa
Waziri wa fedha wa Tanzania , Mhe Mgimwa aliendelea kueleza kuwa, Mkutano huu wa Mawaziri wa Fedha wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola ulifuatia mkutano wa Maafisa wa juu wa Serikali  uliofanyika jana tarehe tisa kwa kuwashirikisha Magavana wa Benki kuu.
“Madhumuni ya msingi ya mkutano huu ni kujadili njia muafaka ambazo zinaweza kutatua matatizo yanayo ukabili uchumi wanchi zetu.” Alisisiza Mgimwa.
Aidha katika mkutano na waandishi wa habari Mhe. Dr. Denzil i. Douglas ambaye ndiye aliyeongoza mkutano huo alisema kuwa, pamoja na mambo yote manne ambayo wameyajadili, wanajitahidi sana kuhakikisha kuwa wanatilia mkazo juu ya kupambana na mtikisiko wa uchumi na kuweka vigezo ambavyo vitasaidia kuzuia kutetereka kwa uchumi wa nchi ambao ni wanachama wa Jumuiya hiyo na kuzuia matatizo ambayo yanaweza kuleta athari kiuchumi.
Mawaziri hao kwa pamoja hawakusita kuzungumzia suala la sekta Binafsi kwani kwa kufanya hivyo kutawawezesha kufikia malengo waliyojiwekea yaani malengo ya maendeleo ya Milenia ya 2015. Aidha Magavana wa Benki kuu walijadili pia changamoto zilizopo za kutokuwa na akiba za kutosha na dhamana katika Benki.
Katibu Mkuu wa sekretarieti  ya  nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola Bw. Kamalesh Sharma akitoa hitimisho kwa waandishi wa habari jioni ya leo alisisitiza sana juu ya uimarishaji wa ushirikiano wa jumuiya hii na zile nchi za kundi la ishirini, G20.Aliongeza  kuwa katika majadiliano yake na Mawaziri hao aliwaambia, “Nategemea nyie kama wanasiasa na mkiwa kama Mawaziri wa Fedha wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, mtakuwa mawakili wazuri wa kuwaelimisha wanasiasa wenzenu na kuendeleza mjadala huu wa kuimarisha uhusiano wetu na nchi za kundi la ishirini (G20),bila hata kukaa kwenye meza na nchi hizo”.Alisisitiza Sharma.
“Mkutano huo ulikuwa na mafanikio na wote kwa pamoja walikubaliana kuyatekeleza yote yaliyoazimiwa”. Alisema Mgimwa.
Mikutano hii ya jumuiya ya Madola inaenda sanjari na Mikutano ya mwaka ya Shirika la Fedha la kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank),ambayo bado inaendelea hapa jijini Tokyo, hadi hapo itakapofikia kilele chake tarehe 14 oktoba.
 Hali ya hewa Jijini hapa ni baridi na manyunyu ya hapa na pale.
Imetolewa na Msemaji Mkuu,
Wizara ya Fedha
Jijini Tokyo- Japani
10 Oktoba 2012.