Pages

Thursday, October 4, 2012

Nchi inakabiliwa na uhaba wa tani 150,000 za sukari


Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima  akifungua mkutano wa wazalishaji wa sukari kutoka nchi za Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Africa(SADC), unaoendelea jijini Dar es Salaam jana.
Mwenyekiti wa wazalishaji wa sukari  (TSPA) kutoka nchi za  SADC Bw. Aswin Rana akizungumza katika mkutano huo jana.
Baadhi ya wazalishaji wa sukari waliohudhuria katika mkutano huo.
…………………………………………………..
Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema nchi inakabiliwa na uhaba wa sukari tani 150,000 kila mwaka kutokana na uwezo wa viwanda hapa nchini kuzalisha tani 350,00 wakati mahitaji ni tani 500,000 kwa mwaka.
Hayo yalisemwa  na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alipokuwa akifungua mkutano wa wazalishaji wa sukari kutoka nchi za Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Africa(SADC), unaoendelea jijini Dar es Salaam
Malima alisema kiasi hicho ambacho ni pungufu imekuwa ngumu kukipata kutoka nchi nyingine kwa kuwa nazo zinahitaji sukari kwa wingi.
“Sisi hatuzalishi sukari kwa kiwango cha kutosha, tuna mahitaji ya sukari tani laki tano kwa mwaka sisi tunazalisha tani laki tatu na hamsini hivyo tuna uhaba wa tani laki moja na nusu ambayo nayo ni ngumu kuipata kutoka kwa wenzetu,”alisema Malima.
Alisema kutokana na hali hiyo Serikali inaweka mkakati ya kutaka uzalishwaji wa sukari ufikie tani milioni moja kwa mwaka ndani ya miaka sita ijayo.
“Kutokana na hilo wadau wa sekta hii ni muhimu wakajipanga ili kuhakikisha lengo hilo linatimia,”alisema na kuongeza;
“Tunaangalia maeneo muhimu ya uzalishaji wa miwa ambayo ndiyo inatumika kutengeneza sukari ili kufanikisha hilo.”
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Wazalishaji wa Sukari Tanzania(TSPA), Balozi Fadhili Mbaga alisema kwa mwaka huu wanategemea kuzalisha sukari kiasi cha tani 320,000 kwa kuwa msimu ni mzuri.
“Mwaka jana tulizalisha tani 80,000 ambayo ilikuwa ni kidogo ila mwaka huu tunatarajia kuzalisha kiasi kikubwa ambacho bado kitakuwa hakitoshi kwa matumizi ya hapa nchini,”alisema Balozi Mbaga.
Alisema hivi sasa nchi za SADC zinazalisha wastani wa tani milioni tano za sukari kwa mwaka ambayo ni asilimia 3 ya uzalishwaji wa sukari duniani. 
Mkutano huo umehudhuriwa na nchi ya Angola, Botswana, Lesotho, Malawi, Mauritius, Musumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

No comments:

Post a Comment