Pages

Thursday, October 11, 2012

POLISI YAUA WATANO KILIMANJARO‏




WATU watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamefariki dunia papohapo baada ya kupigwa risasi  na Polisi katika kijiji cha Kyara  Marangu wilaya ya Moshi  mkoaniKilimanjaro
 
Mbali na Mauaji hayo  pia askari polisi  mwenye namba G.406 Pc Lameck  alijeruhiwa kwa  risasi  katika mguu wa kushoto huku   walinzi watatu wakijeruhiwa kwa mapanga wakati wakijaribu kukoa mali zilizoporwa katika duka hilo .
 
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro Bw.Robert  Boaz amethibitisha kutokea kwa tukio hilo  majira ya saa 7 usiku  wa kuamkia leo baada ya kuvamia duka la Bw. Gaudence Temu na kuiba vifaa mbalimbali vya ujenzi.
 
Akielezea mazingira ya tukio hilo  kamanda Boaz alisema kundi la majambazi watano walivamia dukani  kwa Gaudence Temu na kumjeruhi kwa sime mlinzi aitwaye Hamis Juma (25) na kisha kuiba.
 
Alisema kufuatia tukio hilo  walinzi wa sungusungu  Richard Temu na Erick Yuda walijitokeza ili kutoa msaada lakini nao walishambuliwa kwa mapanga na kujeruhiwa na wote wamelazwa katika hospitali ya Kilema.
 
Kwa mujibu wa kamanda Boaz baada ya tukio hilo taarifa za uvamizi zilifikishwa polisi  na askari wa doria walikwenda haraka eneo la tukio kutoa msaada na kuanza kuwasaka majambazi hao ambao walitokomea mara baada ya tukio hilo.
 
Alisema ufuatiliaji wa kina ulifanyika na kubaini maficho ya majambazi hao ambayo ni nyumba ya mmoja wao iliyopo kijiji cha Kyara eneo la Marangu, ambapo askari walikwenda  na baada ya kufika waliwataka wafungue mlango  na kujisalimisha lakini hawakutaka hadi Bomu la machozi lilipotupwa  katika nyumba hiyo.
 
Alisema mara baada ya Bomu la machozi kutupwa majambazi hao walitoka nje  huku wakirusha risasi  ambapo chembechembe za risasi zilimjeruhi  skari mmoja ambaye  ni Pc Lameck  kwenye mguu wa kushoto.
 
“Askari nao walijibu mapigo na kufanikiwa kuwapiga risasi na kuwaua  majambazi watano waliojaribu kutoroka kutoka kwenye nyumba hiyo”alisema kamanda.
 
Aidha aliwataja majambazi hao kuwa ni Paul Baltazari Bahati (25) ambaye ni mwenye nyumba, Remius Msambure kwa jina maarufu mreno (30) ,Focus Daud Mtui ( kwa jina maarufu Kisinja (35) wote wakazi w kijiji cha Kitowo Marangu,Elia  aliyetambulika kwa jina moja mmasai  mkazi wa kijiji cha Msitu wa Tembo na mmoja bado hajatambulika.
 
Kamanda alisema katika eneo la tukio  ilikutwa bunduki moja aina ya Shortgun greener yenye  No. 858356 na risasi nne, maganda ya risasi ambapo bunduki hiyo iliibwa Tarehe septemba 15 mwaka huu katika kijiji cha Chemchem wilaya ya Moshi kwa  Bw. Kribia Bwanakule Mmari.
 
Vingine ni Pistol aina ya Browning ambayo imefutwa namba  na risasi mbili,Risasi 10 za bunduki aina ya SMG,Mapanga,sime,yenye damu, Brief case yenye mabomba ya sindano,sindano, uzi wa kushonea majeraha hospitali,zana mbalimbali za kuvunjia pamoja na mali mbalimbali za wizi.
 
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa moshi wamepongeza hatua ya jeshi hilo na kusema kuwa majambazi hao wamekuwa kero katika kijiji hicho kwa muda mrefu hali ambayo ilikuwa ikiwanyima usingizi kwa kuhofia kuvamiwa.

No comments:

Post a Comment