KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuchunguza mauaji ya mwanahabari, Daudi Mwangosi, imekamilisha kazi yake, huku ikitoa siri nzito.
Siri hiyo ambayo huenda ikasababisha baadhi ya vigogo wa polisi kupoteza kazi, itawekwa hadharani katika mkutano wa waandishi wa habari Jumanne ijayo, mbele ya kamati hiyo na Waziri Nchimbi mwenyewe.
Tayari kamati hiyo iliyofanya kazi kwa siku 30, imekabidhi ripoti yake kwa Dk. Nchimbi jana, kumpa fursa ya kuipitia kabla ya ukweli kuhusu mauaji hayo kuwekwa hadharani.
Ripoti hiyo ilikabidhiwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Theophil Makunga ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communication.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makunga alisema kamati yake ilifanya ziara mkoani Iringa na kufanya mahojiano na wadau mbalimbali mkoani humo na jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo jana, Dk. Nchimbi kupitia taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari, ameahidi kuwa yeye pamoja na kamati hiyo, watafanya kikao na waandishi wa habari kueleza kilichobainishwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa Wizara hiyo, Isaac Nantanga, Nchimbi mbali na kupokea ripoti hiyo aliishukuru kamati kwa kazi waliyoifanya.
Ripoti ya kamati hiyo imekabidhiwa ikiwa ni takribani zaidi ya mwezi mmoja tangu mwanahabari huyo alipouawa kinyama na polisi Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi wakati polisi walipovamia na kutawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho.
Mazingira ya kifo cha Mwangosi yamesababisha uhasama mkubwa baina ya Jeshi la Polisi na wanahabari ambao katika baadhi ya mikoa wameamua kususia kazi za jeshi hilo.
Mgogoro huo ulisababisha Nchimbi afikie hatua ya kuunda kamati hiyo baada ya siku tatu tangu kutokea kwa mauaji hayo ili kubaini utata wa kifo hicho.
Kamati hiyo yenye watu watano iliwashirikisha Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Steven Ihema, Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike.
Wengine ni mtaalamu milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo pamoja na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Isaya Mungulu.
Dk. Nchimbi aliiagiza kamati hiyo kufanya kazi yake kwa siku 30 na kukabidhi ripoti kwake na kueleza umma chanzo cha tukio hilo.
Kamati hiyo ilipewa hadidu za rejea sita huku Nchimbi akiahidi kwamba askari watakaobainika kuhusika na tukio hilo, watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Hadidu za rejea ni pamoja na maswali kadhaa kuhusu chanzo cha kifo cha Mwangosi.
Nyingine ni ile inayotokana na kuwepo kwa taarifa kwamba kuna uhasama kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa na kama kuna waandishi watatu wa habari wanatafutwa na
polisi.
Hadidu nyingine ni kujibu maswali kama nguvu iliyotumika katika kukabiliana na tukio lile ilikuwa kubwa kupita kiasi na je, kuna taratibu za kukata rufaa kwa chama kinachodhani hakikutendewa haki na Jeshi la Polisi?
Pia aliiagiza kamati hiyo ichunguze kama kuna tatizo kwa vyama vya siasa kwamba, havina mahusiano mazuri na Jeshi la Polisi.
Hata baada ya kamati hiyo kuundwa, waandishi wa habari katika baadhi ya mikoa, ikiwamo Dar es Salaam waliongoza maandamano ya kulaani mauaji ya mwanahabari mwenzao.
Source:tanzania daima
TASHICO YAFAFANUA MELI MV SERENGETI KUZAMA ZIWA VICTORIA
-
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
KAMPUNI ya Meli Tanzania (TASHICO) imefafanua tukio la kuzama kwa meli ya
MV Serengeti katika Bandari ya Mwanza Kusini,Ziwa V...
6 hours ago
No comments:
Post a Comment