KAMATI
iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi,
kuchunguza mauaji ya mwanahabari, Daudi Mwangosi, imekamilisha kazi
yake, huku ikitoa siri nzito.
Siri hiyo ambayo huenda
ikasababisha baadhi ya vigogo wa polisi kupoteza kazi, itawekwa
hadharani katika mkutano wa waandishi wa habari Jumanne ijayo, mbele ya
kamati hiyo na Waziri Nchimbi mwenyewe.
Tayari kamati hiyo
iliyofanya kazi kwa siku 30, imekabidhi ripoti yake kwa Dk. Nchimbi
jana, kumpa fursa ya kuipitia kabla ya ukweli kuhusu mauaji hayo kuwekwa
hadharani.
Ripoti hiyo ilikabidhiwa na Makamu Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Theophil Makunga ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa
Mwananchi Communication.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makunga
alisema kamati yake ilifanya ziara mkoani Iringa na kufanya mahojiano na
wadau mbalimbali mkoani humo na jijini Dar es Salaam.
Mara baada
ya kukabidhiwa ripoti hiyo jana, Dk. Nchimbi kupitia taarifa
iliyosambazwa kwa vyombo vya habari, ameahidi kuwa yeye pamoja na kamati
hiyo, watafanya kikao na waandishi wa habari kueleza kilichobainishwa.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa Wizara hiyo, Isaac
Nantanga, Nchimbi mbali na kupokea ripoti hiyo aliishukuru kamati kwa
kazi waliyoifanya.
Ripoti ya kamati hiyo imekabidhiwa ikiwa ni
takribani zaidi ya mwezi mmoja tangu mwanahabari huyo alipouawa kinyama
na polisi Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo wilayani
Mufindi wakati polisi walipovamia na kutawanya wafuasi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa wakifungua tawi la chama
hicho katika kijiji hicho.
Mazingira ya kifo cha Mwangosi
yamesababisha uhasama mkubwa baina ya Jeshi la Polisi na wanahabari
ambao katika baadhi ya mikoa wameamua kususia kazi za jeshi hilo.
Mgogoro
huo ulisababisha Nchimbi afikie hatua ya kuunda kamati hiyo baada ya
siku tatu tangu kutokea kwa mauaji hayo ili kubaini utata wa kifo hicho.
Kamati
hiyo yenye watu watano iliwashirikisha Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu,
Steven Ihema, Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili
Mtambalike.
Wengine ni mtaalamu milipuko kutoka Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo pamoja na Kamishna Msaidizi wa
Jeshi la Polisi, Isaya Mungulu.
Dk. Nchimbi aliiagiza kamati hiyo kufanya kazi yake kwa siku 30 na kukabidhi ripoti kwake na kueleza umma chanzo cha tukio hilo.
Kamati
hiyo ilipewa hadidu za rejea sita huku Nchimbi akiahidi kwamba askari
watakaobainika kuhusika na tukio hilo, watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Hadidu za rejea ni pamoja na maswali kadhaa kuhusu chanzo cha kifo cha Mwangosi.
Nyingine
ni ile inayotokana na kuwepo kwa taarifa kwamba kuna uhasama kati ya
Jeshi la Polisi na waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa na kama kuna
waandishi watatu wa habari wanatafutwa na polisi.
Hadidu
nyingine ni kujibu maswali kama nguvu iliyotumika katika kukabiliana na
tukio lile ilikuwa kubwa kupita kiasi na je, kuna taratibu za kukata
rufaa kwa chama kinachodhani hakikutendewa haki na Jeshi la Polisi?
Pia aliiagiza kamati hiyo ichunguze kama kuna tatizo kwa vyama vya siasa kwamba, havina mahusiano mazuri na Jeshi la Polisi.
Hata
baada ya kamati hiyo kuundwa, waandishi wa habari katika baadhi ya
mikoa, ikiwamo Dar es Salaam waliongoza maandamano ya kulaani mauaji ya
mwanahabari mwenzao. Source:tanzania daima
No comments:
Post a Comment