MADAI YA RUSHWA YATAWALA, MALISA, SHIGELLA, BASHE, NYALANDU WATUHUMIWA, MAKONDA ATOA KAULI NZITO.
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni
akimpongeza, Khamis Sadifa Juma baada ya kutangazwa kuwa Mwenyekiti Mpya
wa Umoja wa Vijana wa CCM UVCCM, mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa
kazi ya kuhesabu kura.
Neville Meena, Dodoma.
MATOKEO
ya uchaguzi wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
yametangazwa jana huku kukiwa na harakati za kuyapinga kwa madai ya
ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Kati ya
mambo yaliyotajwa kupindisha taratibu za uchaguzi huo uliofanyika juzi
ni kile kilichoelezwa kuwa ni kutawaliwa na vitendo vya rushwa.
Baada ya
Msimamizi wa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi kutangaza matokeo, baadhi ya vijana
waliyapinga na kuanza kukusanya saini 340 ili kuyapinga.
Katika
kuonyesha kutoridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi, baadhi ya wajumbe
walibeba mabango yenye ujumbe wa kutokubaliana na matokeo, mbele ya
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed
Shein baada ya kumaliza kufunga mkutano huo.
Moja ya
bango hilo lilikuwa na maneno: “Jumuiya si ya Lowassa na wafuasi wake
(Benno, Bashe, Zungu, Zabein…..) hivyo jumuiya itakuwa na kambi mbili ya
kwanza jukwaani na kambi ya mezani.”
Bango jingine lilisomeka: “Jumuiya imara hujengwa na uchaguzi wa haki na siyo rushwa za Bashe, Benno na Zungu.”
Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa
kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kambi yake imekuwa
ikitajwa kuwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi wa ndani wa CCM.
Kwa
tafsiri ya mabango hayo, Benno (Malisa) alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa
UVCCM aliyemaliza muda wake, Bashe (Hussein) naye alikuwa ni Mjumbe wa
Baraza Kuu la jumuiya hiyo ambaye amemaliza muda wake.
Maofisa
usalama na walinzi wa jumuiya hiyo ambao walikuwa wakijaribu
kuwanyang’anya vijana hao mabango walishindwa, hivyo kulazimika kusubiri
dakika kama tano hivi hadi msafara wa Dk Shein ulipoondoka walipowatoa
nje ya eneo la ukumbi wa mkutano.
Tukio
hilo lilizua tafrani baada ya walinzi hao kuwanyanyua juujuu vijana
wawili kati ya sita waliokuwa na mabango, huku wengine wakionekana
kutaka kuwapiga lakini polisi waliingilia kati na kuwatoa nje.
Baadaye
polisi waliondoka na vijana watatu katika tukio ambalo lilikuwa
likifuatiliwa kwa karibu na baadhi ya wagombea ambao walishindwa katika
nafasi mbalimbali za uongozi wa UVCCM.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhOy0SRGxIES3_lsnuYKOT6SjBT15Gv9t9TNN8H_L-6PAmPiy1YPQ9syPiB9ZNq6I2FOlufpZ7U9HJXbJBsuJl4LHqorduq5vr604Mgh32U-xl-iFmuo3CRADYXO5D52lvtmLj1xN55nPo/s640/mali.jpg)
Mjumbewa
Kamati Kuu ya CCM, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed
Shein, (Kulia), akishuhudia wakati Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa
Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), aliyemaliza muda wake, Benno
Malisa, (Wapili kushoto), akimpongeza mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo
aliyechaguliwa kwenye mkutano mkuu uliofanyika jana Jumanne mjini
Dodoma, Khamis Sadifa Juma.
Vijana walalama.
Mapema
jana asubuhi, kundi la vijana kutoka mikoa mbalimbali walikutana na
waandishi wa habari na kulalamika kwamba rushwa ilitawala huku
wakiwatuhumu viongozi wa UVCCM na baadhi ya makada wa chama hicho kwa
kuhusika na vitendo hivyo.
Waliotajwa ni pamoja Malisa, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, Bashe na mtoto wa Lowassa, Fredy.
“Kama
Rais Jakaya Kikwete kweli yuko makini na kauli zake ni za dhati, basi
atengue matokeo ya uchaguzi huu maana kanuni zimekiukwa na kusema kweli
rushwa ilitawala.
Atumie
nafasi yake kurejesha hadhi ya chama, huu uchaguzi ni batili,” alisema
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka Morogoro, Augustine Matefu.
Walidai
kuwa Bashe ndiye aliyekuwa mratibu wa uingizaji wa fedha katika eneo la
mkutano ambazo zilitumika kugawanywa kwa wajumbe na kwamba Malisa na
Shigela waligawa Sh1 milioni kwa viongozi wa mikoa kama hatua ya
kumpigia kampeni mmoja wa wagombea walioshinda.
Kada
mwingine, Livamba Adinan Selemani alisema: “Vijana kweli tumempuuza
Rais, kweli mtu ambaye hana hela hawezi kupata uongozi UVCCM, kwa maana
nyingine nchi yetu inakwenda pabaya. Watu wachache wenye fedha wanaweza
kuamua kufanya wanachotaka, hivyo ndivyo uchaguzi wetu wa vijana
ulivyokuwa.”
Mjumbe
mwingine, Kichanta Selemani alisema malalamiko ya viongozi wa UVCCM
kuwapendelea baadhi ya wagombea yalifikishwa kwa Lukuvi lakini hakuna
hatua zilizochukuliwa.
Wakati
makada hao wa CCM wakizungumza na waandishi wa habari, lilitokea kundi
jingine la makada wa chama hicho ambao walianza kuzozana na wenzao
wakisema kuwa malalamiko yao yanatokana na kushindwa na kwamba walitaka
kutumia: “Viongozi wa ngazi za juu za CCM” kuwachagulia vijana viongozi.
Kundi
hilo la pili lilidai kuwa katika uchaguzi huo kundi hilo la kwanza ndilo
lililohonga fedha na kumtaja Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu kwamba alikuwa akiwashawishi wajumbe kwa fedha kumchagua
mmoja wa wagombea.
Akizungumzia tuhuma hizo, Nyalandu alisema kupitia ujumbe wa simu yake ya mkononi:
“Mimi siyo mjumbe wala mgombea na wala sihusiki kwa lolote.
Nilikwenda
ukumbini na waziri mwenzangu na baadaye tukaondoka pamoja. Hao ni
waongo wakubwa na wazushi wachache wanaonunua haki.”
Hakuna
mtu yeyote niliyeongea naye wala kutoa hela yoyote kwa sababu zozote
zile na tulikuwa ukumbini baadaye nje wote pamoja (na waziri). Shame to
them who lie (aibu kwao wanaosema uongo) na wataje majina yao
tuyasikie.”
Alimtaja
Waziri aliyekuwa naye kuwa ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba
kwa lengo la kuwasalimia vijana ambao walikuwa wakiendelea na mkutano
wa uchaguzi.
Watuhumiwa wanena
Kwa
nyakati tofauti, wakijibu tuhuma hizo watuhumiwa wote walikanusha
kuhusika kutoa rushwa na kuwataka wanaolalamika kupeleka ushahidi wao
Takukuru na kufikisha malalamiko hayo katika vikao vya ulinzi na maadili
vya CCM.
Shigela
kwa upande wake, akizungumza na waandishi wa habari alisema kinachotokea
sasa kuhusu tuhuma hizo kilitarajiwa kwani ni kawaida watu
wanaposhindwa katika uchaguzi kutoa malalamiko hata kama hawana ushahidi
wa tuhuma husika.
Shigela
alikanusha yeye na Malisa kutoa fedha kwa viongozi wa mikoa akisema kwa
nafasi yake asingeweza kupata fursa ya kufanya hivyo kwani alikuwa
mratibu mkuu wa uchaguzi kuhakikisha kila jambo linakwenda sawa.
“Kama
kuna watu hawakuridhika kuna taratibu za chama inabidi zifuatwe, kwa
mujibu wa taratibu zetu kuna siku 14 za malalamiko na hizo mtu anaweza
kuzitumia kuandika malalamiko yake na yapelekwe kwa viongozi wahusika
ili wachuke hatua,” alisema Shigela na kuongeza:
“Vinginevyo
taratibu za chama haziruhusu kutoa au kupokea rushwa kwa namna yeyote,
kwa hiyo kama mtu anadhani ana uwezo aitumikie jumuiya popote pale alipo
kwa sababu wote hatuwezi kuwa viongozi kwa pamoja.”
Kwa
upande wake, Malisa alisema: “Nimefanya kazi yangu na kutekeleza wajibu
wangu kwa ukamilifu, kama kuna jambo lolote ambalo linahusu UVCCM, basi
kamuulizeni mwenyekiti wa jumuiya maana yupo.”
Bashe
alikanusha kuhusika na vitendo vya rushwa na kuwataka wanaotoa madai
hayo, kama wana ushahidi waupeleke Takukuru au kufikisha suala hilo
katika vikao vya chama hicho.
“Waambieni kwamba wasilete siasa za shule za sekondari UVCCM, maana kama wangeshinda ni dhahiri kwamba wasingelalamika.
Ninawapa
ushauri wa bure, kwanza kama wana ushahidi wa madai hayo kwamba mimi
Hussein nimetoa rushwa, basi wapeleke ushahidi wao Takukuru lakini pia
ndani ya chama tunayo Kamati ya Maadili na Usalama wapeleke malalamiko
yao huko ili yafanyiwe kazi.”
Alisema hawezi kujihusisha na rushwa kwani hata Rais Kikwete katika hotuba ya ufunguzi alikemea vitendo hivyo.
Fredy akizungumza kwa simu alisema:
“Tuhuma
hizo siyo za kweli kwani mimi licha ya kwamba nilipata barua ya mwaliko
wa kuhudhuria mkutano huo sikuenda Dodoma kutokana na kubanwa na kazi.
“Kwanza
mimi si mjumbe wa mkutano mkuu japokuwa ni Katibu wa Uhamasishaji wa
Mkoa wa Arusha. Nilipata mwaliko lakini sikuweza kufika huko (Dodoma)
nimetingwa na kazi nyingi,” alisema.
Matokeo ya uchaguzi
Lukuvi alimtangaza Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamisi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM baada ya kupata kura 483.
Sadifa
alimshinda Rashid Simai Msaraka aliyepata kura 263, wakati mgombea
mwingine Lulu Msham Abdallah licha ya kujitoa katika kinyang’anyiro
hicho muda mfupi kabla ya kura kupigwa, alipata kura nane.
Katika
nafasi ya Makamu Mwenyekiti Mboni Muhita alishinda katika duru ya pili
baada ya kupata kura 489 na kumshinda, Paul Makonda aliyepata kura 241.
Katika
duru ya kwanza, Mboni alikuwa amepata kura 361 na Makonda kura 206, huku
mgombea mwingine Ally Salum Hapi akipata kura 179.
Uchaguzi huo ulirudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura kama kanuni zinavyotaka.
“Sheria kushindwa kwa heshima kuliko kushinda kwa fedheha.”
Makonda
aliyekuwa akizungumza kwa hisia jukwaani alisema ikiwa UVCCM wanataka
kujenga taasisi yenye nguvu na inayoaminika, lazima wahakikishe
wanajiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaua demokrasia.
“Uchaguzi
tulioufanya hatukumchagua Sadifa wala Mboni, bali tumechagua uongozi wa
aina ya jumuiya tunayoitaka, sasa tutarajie jumuiya hiyo…. kama
sikueleweka historia itakuja kutuambia maana ya maneno haya,” alisema
Makonda na kuongeza:
“Kama
kuna mtoto wa maskini, mtoto wa mkulima kama mimi amechagua au kupiga
kura yake kwa sababu ya rushwa, basi ajue amepanda mbegu maishani
mwake.”
Baada ya
Makonda kutoa kauli hizo alishuka jukwaani na kwenda moja kwa moja nje
ya ukumbi ambako baadhi ya wapambe wake walimfuata na kuanza kulia
machozi.
Baadhi
yao walisikika wakisema kwamba UVCCM wameisaliti demokrasia kutokana na
nguvu ya fedha. Hata hivyo, Makonda alikuwa akiwafariji kwa kuwaambia
wasife moyo.
No comments:
Post a Comment