WAREMBO 30 kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini
wanatarajiwa kuingia kambini leo kwenye hoteli ya Giraffe kwa ajili ya kuanza
maandalizi ya kushiriki shindano la urembo la Taifa 'Redd's Miss Tanzania 2012'
litakalofanyika Novemba 3 kwenye ukumbi wa hoteli ya Ubungo Plaza hapa jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini, Mkurugenzi wa Kampuni
ya Lino Agency International, Hashim Lundenga alisema kuwa warembo wote walishapewa
taarifa za kuripoti kambini leo na mara baada ya kuwasili watapewa taratibu za
kambi hiyo.
Lundenga aliwataka washiriki hao kuhakikisha
wanawasili asubuhi mapema katika ofisi za Kamati ya Miss Tanzania kama
walivyoambiwa ili wapelekwe pamoja katika hoteli hiyo iliyoandaliwa kwa ajili
ya kambi yao ya mwezi mzima.
Alisema warembo wakiwa katika kambi ya Redd's
Miss Tanzania watafundishwa mambo mengine muhimu katika maisha yao ambayo
yatawafanya wajiandae kuwa wanawake walio na maendeleo na watakaokuwa tayari
kuongoza familia zao.
Alisema pia baada ya kumpata mshindi atakapewa
mapumziko ya miezi miwili na baadaye ataanza maandalizi ya kujiandaa
kuiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia ya mwakani.
Alisema kuwa licha ya kuwepo na changamoto
mbalimbali katika mashindano hayo, anawapongeza mawakala kwa kazi ya kusaka
warembo ambao wengi wao waliofanikiwa kufuzu fainali hizo ni wanafunzi wa Vyuo
vya Elimu ya Juu.
No comments:
Post a Comment