Pages

Saturday, November 3, 2012

IGP MWEMA AMTEUA MRITHI WA RPC BARLOW.



IGP SAIDI MWEMA.

Raymond Kaminyoge
INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema amemteua Ernest Mangu
 kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, kuziba pengo lililoachwa na 
Liberatus Barlow aliyeauawa kwa risasi hivi karibuni.

Hata hivyo, katika uteuzi huo ulioambatana na uhamisho wa baadhi ya makamanda wa mikoa na vikosi vingine vya jeshi hilo, IGP Mwema
 hakumgusa Kamanda wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda ambaye 
kumekuwa na shinikizo la kutaka awajibishwe kutokana na mauaji ya
 mwandishi wa habari, Daud Mwangosi mkoani huo yaliyotokea 
Septemba 2, mwaka huu.

Kamanda Barlow aliuawa Oktoba 13, mwaka huu baada ya kupigwa risasi
 na watu katika tukio ambalo chanzo chake bado hakijafahamika wakati 
akitoka katika kikao cha harusi. Kabla ya kuhamishiwa Mwanza, Mangu
 alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Msemaji wa
 Jeshi la Polisi, Advera Senso, Kamanda wa Mkoa wa Polisi Temeke, David
 Misime anahamishiwa Mkoa wa Dodoma kuchukua nafasi ya,
 Zelothe Stephen anayestaafu.

Katika uhamisho huo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege,
 Ulrich Matei amehamishiwa Pwani kuchukua nafasi ya Mangu.

Taarifa hiyo ilisema Engelbert Kiondo aliyekuwa Idara ya Upelelezi makao 
makuu, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke.

Kamanda mpya wa Kikosi cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia 
(Tazara), anakuwa Rashid Seif ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa pia
 Idara ya Upelelezi makao makuu. Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema 
kamanda wa Tazara amepangiwa kazi gani na juhudi za kumpata 
Senso kutoa ufafanuzi hazikufanikiwa.

Nafasi ya Matei Viwanja vya Ndege imechukuliwa na Deusdedit Kato ambaye
 kabla ya uteuzi huo alikuwa makao makuu ya jeshi hilo.

Katika mabadiliko hayo, Kamanda wa Kikosi cha Ufundi, Shaban Hiki
 anahamia Makao Makuu ya Polisi na nafasi yake inachukuliwa na Lucas 
Mkondya aliyekuwa makao makuu.

Mabadiliko hayo pia yamemhusisha aliyekuwa Ofisa Mnadhimu wa 
Kikosi cha Usalama Barabarani, Johansen Kahatano anakwenda kusimamia
 Mradi wa Smatter Traffic na nafasi yake imechukuliwa na Kamanda wa 
Kikosi cha Usalama Barabani (RTO) Mkoa wa Pwani, Swalehe Mbaga.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uhamisho huo pia umewahusisha baadhi ya 
wakuu wa operesheni wa mikoa, wakuu wa vikosi vya kutuliza ghasia, 
wakuu wa polisi wa wilaya na wakuu wa upelelezi wa wilaya.
Jeshi hilo limesema kwamba uhamisho huo ni wa kawaida kwa mujibu 
wa kanuni, taratibu na miongozo yake.

No comments:

Post a Comment