Pages

Tuesday, November 27, 2012

Rufaa ya Lema kuanza Des.4




HATIMAYE Mahakama ya Rufani Tanzania, Desemba 4, itaanza kusikiliza rufaa ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA).
Lema alikata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa Aprili 5, mwaka huu, na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, chini ya Jaji Gabriel Rwakibarila, ambaye alikubaliana na hoja za walalamikaji, hivyo kumvua ubunge.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufani, jopo la majaji watatu watakaosikiliza rufaa hiyo, ni Jaji Salum Massati, Natharia Kimaro na Bernad Luanda ambao kikao chao kitaketi jijini Dar es Salaam, kuanzia saa tatu asubuhi.
Kupangwa kwa tarehe ya kuanza kusikiliza rufaa hiyo kumekuja baada ya Lema kuwasilisha rufaa yake upya ambayo ameifanyia marekebisho kama alivyoamriwa na mahakama hiyo Novemba 8, mwaka huu.
Mahakama hiyo ilikataa ombi la wajibu maombi katika rufaa hiyo waliotaka mahakama iifute rufaa ya Lema kwa sababu ina mapungufu badala yake ikiri kubaini mapungufu hayo.
Hata hivyo katika uamuzi wake kwenye pingamizi hilo, mahakama hiyo ikasema mapungufu hayo hayawezi kuifanya ifikie uamuzi wa kuifuta rufaa ya Lema kwani mapungufu hayo yalifanywa na watendaji wa mahakama.
Hivyo mahakama hiyo ilimpatia Lema siku 14 kuanzia siku hiyo awe amewasilisha upya rufaa yake aliyoifanyia marekebisho.
Aprili 5, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitoa hukumu yake na kumvua ubunge Lema kufuatia kesi iliyofunguliwa na wanachama watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Lema alikata rufaa Mahakama ya Rufani, kupitia kwa wakili wake Method Kimomogoro kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, akitoa hoja 18 za kupinga hukumu hiyo.
SOURCE TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment