Pages

Tuesday, November 27, 2012

Wakuu wa wilaya wakimbia vituo PINDA ABAINI ATISHIA KUWATIMUA KAZI




WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewaagiza wakuu wa wilaya mpya zote nchini waishi kwenye maeneo ya makao makuu ya wilaya zao vinginevyo atawachukuliwa hatua za kuachishwa kazi.
Agizo hilo alilitoa jana wakati akiwahutubia wananchi kwenye sherehe ya uzinduzi wa mkoa mpya wa Katavi iliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kashaulili.
Pinda alisema wako baadhi ya wakuu wa wilaya mpya ambao toka wachaguliwe wamekuwa wakiishi nje ya wilaya zao.
Alisema wakuu wa wilaya ambao wanaona hawawezi kukaa kwenye wilaya zao ni vizuri wakawapisha watu wengine kwani wapo Watanzania wengi wanazihitaji nafasi hizo.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa kitendo cha wakuu wa wilaya mpya kutoishi kwenye maeneo yao kinasababisha washindwe kusimamia ipasavyo maendeleo ya wilaya zao.
“Kama hamuishi kwenye wilaya zenu mnategemea nani atakayesimamia maendeleo ya wilaya zenu?” alihoji.
Aliwataka wakuu wa mikoa kuhakikisha wakuu wa wilaya wote wanaishi kwenye wilaya zao na si vinginevyo.
Pinda aliwaagiza wakuu wa mikoa kutoa taarifa kwake kama kutakuwa na mkuu wa wilaya ambaye anaishi nje ya wilaya yake ili aweze kumchukulia hatua.

No comments:

Post a Comment