Pages

Thursday, November 1, 2012

Utoro Huu wa Wabunge Bungeni Kamwe Haukubaliki


  'Tunaamini, ofisi ya Spika, Anne Makinda na Katibu wake, Dk Thomas Kashillilah wataliangalia hili upya na uwajibikaji wa kila mbunge ambao baadhi yao wakati mwingine wamekuwa wakipigiwa kelele na wapiga kura wao kwamba wanashindwa kuwawakilisha ipasavyo.'

LICHA ya ukweli kwamba Bunge ni taasisi iliyo huru na mojawapo ya mihimili mikuu mitatu ya Dola, kwa Tanzania, mhimili huu kwa siku za karibuni utendaji wake umekuwa ukitia shaka.

Pamoja na ukweli kwamba Bunge letu linatakiwa kujiendesha kwa uhuru bila kuingiliwa, lakini tukiwa sehemu ya jamii, tunao wajibu wa kulikosoa pale linapokuwa limekwenda kombo na kulipongeza na kulishauri kadri inavyowezekana.


Bunge letu la sasa ambalo linaundwa na vijana wasomi wazuri pamoja na wakongwe wenye uzoefu, linakutana kwa mjini Dodoma tangu juzi.


Hata hivyo, lilianza vibaya kwani katika kikao chake cha kwanza cha juzi Jumanne, kililazimika kuahirishwa kulingana na kanuni za kazi zinazosimamia chombo hiki kikuu cha kutunga sheria kutokana na kutotimia akidi ya wabunge wanaotakiwa kupitisha azimio au hata muswada wa sheria, ambao ni nusu ya wabunge wote 357.


Ingawa wabunge wengi wanaweza kujitetea kwa uzembe huo, tayari kitendo hicho ambacho kimetafsiriwa na wengi kama utoro kilisababisha shughuli iliyopangwa siku ile, yaani ya kupitisha Azimio la Bunge la Marekebisho ya Pili ya Ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya, Afrika, Caribean na Pacific (ACP), kukwama.


Hatukufurahishwa na kitendo hiki hasa ikizingatiwa kwamba kimefanyika kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi minne. Mara ya kwanza wabunge kukwamisha shughuli za Bunge ilikuwa wakati wa kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika katika Mkutano wa Nane.


Bajeti hiyo ilikwama wiki moja tu tangu Spika wa Bunge, Anne Makinda kukemea tabia ya utoro akisema ilikuwa imekithiri.Kitendo cha utoro wa mara kwa mara cha wabunge wetu, kikionyesha ama kujisahau, kukosa umakini au wakati mwingine utovu wa nidhamu.

Tumekuwa tukieleza mara zote kwamba inafaa kanuni zote zinazosimamia uendeshaji wa chombo hiki zitazamwe upya na ikiwezekana kuwe na hatua zikiwamo za kinidhamu kwa mbunge mmoja mmoja anayekiuka kanuni hizi ikiwamo kutohudhuria mikutano na vikao ipasavyo.

Tunashauri, utaratibu wa kuwapa ruhusa wabunge kuondoka Dodoma kwa shughuli zao binafsi unafaa nao uangaliwe upya, kwa umakini, hasa kama ndio unaotoa nafasi kwao kuwa watoro katika vikao ambavyo gharama zake pia ni kubwa mno.

Ni jambo lisilokubalika kuona kodi za wananchi wa kawaida wa Tanzania, yaani wakulima na wafanyakazi na kidogo wafanyabiashara ambazo hulipa mishahara au posho nono za wabunge wetu zinaachwa kutumika vibaya kwa watu ambao hawaoni sababu ya kuhudhuria vikao.

Tunaamini, ofisi ya Spika, Anne Makinda na Katibu wake, Dk Thomas Kashillilah wataliangalia hili upya na uwajibikaji wa kila mbunge ambao baadhi yao wakati mwingine wamekuwa wakipigiwa kelele na wapiga kura wao kwamba wanashindwa kuwawakilisha ipasavyo.


Tunashauri Bunge liangalie pia kanuni na kuratibu ziara zote ambazo zimekuwa wakati mwingine zikiruhusiwa kufanywa na wabunge wakati mikutano ya Bunge ikiendelea Dodoma kwani baadhi yao wameondoka huko na kwenda kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Vinginevyo, mienendo ya namna hii ya wabunge wetu kutoonekana bungeni na wananchi kupitia kwenye luninga kuona viti vingi vikiwa tupu, vinatoa picha mbaya si kwao tu, bali taasisi nzima.

Wabunge wanapaswa kufahamu kwamba wapiga kura wao wanawafuatilia, baada ya kuwachagua wanategemea kuwaona wakiwajibika ipasavyo bungeni kwa maana ya kuhudhuria vikao na kutoa hoja zenye mustakabali mwema kwa ustawi wao na taifa lao na siyo kufanya shughuli kinyume cha hapo na wanapofika bungeni kuanza kuzomeana na kupigana vijembe.


Tunapendekeza, iwe mwiko kwa mbunge yeyote kuondoka Dodoma hasa wakati wa vikao vya Bunge bila sababu maalumu, na zinazokubalika kama vile za kiafya, kufiwa au zile ambazo haziwezi kutiliwa shaka au kuhojiwa na yeyote. Umefika wakati pia kwa ratiba ya mikutano minne ya Bunge ya kila mwaka kupangwa vizuri ili isiingiliane pasipo sababu za msingi na majukumu mengine ya kitaifa kama vile ziara za viongozi wakuu na mambo mengine kama hayo.



*Uchambuzi kutoka Mwananchi

No comments:

Post a Comment