Pages

Friday, November 30, 2012

ZANZIBAR YAIKALISHA RWANDA NAMBOOLE


Khamis Mcha ‘Vialli’ akiruka kushangilia baada ya kufunga bao la kwanza. Kushoto ni Jaku Juma.

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
MABAO mawili ya kiungo wa Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’ usiku huu yameipa Zanzibar ushindi wa 2-1 dhidi ya Rwanda, katika mchezo wa Kundi C, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge uliofanyika kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala.
Kwa ushindi huo, Zanzibar Heroes imefufua matumaini ya kwenda Robo Fainali ya michuano hii, ikipanda kileleni mwa Kundi hilo, kwa pointi zake nne, Rwanda ikishuka nafasi ya pili kwa pointi zake tatu, sawa na Malawi, wakati Eritrea inashika mkia kwa pointi yake moja.
Vialli alifunga mabao yake moja kila kipindi, la kwanza dakika ya sita na la pili dakika ya 61, yote akionyesha yeye ni fundi na mwenye akili na maarifa ya soka kutokana na kutulia na kumtungua kipa hodari kabisa katika ukanda huu, Jean Claude Ndoli.
Rwanda ilipata bao lake kupitia kwa Dadi Birori dakika ya 79, ambaye aliingia uwanjani dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Tumaine Ntamuhanga.
Mchezo wa leo kama ulivyokuwa mchezo wa kwanza kati ya Malawi na Eritrea ulitibuliwa na mvua iliyoharibu mandhari ya Uwanja wa Mandela, hivyo haikuwa wa ufundi zaidi ya ‘butua butua’.
Nahodha wa Zanzibar, Nadir Heroub ‘Cannavaro’ alisema baada ya mechi hiyo kwamba wamefuta makosa yao ya mchezo wa kwanza na sasa Wazanzibari wasubiri Kombe, wakati Haruna Niyonzima wa Rwanda, alilalamikia Uwanja mbovu leo kuwasababisha kucheza ovyo.  
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Zanzibar kilikuwa; Mwadini Ally, Nassor Masoud ‘Cholo’, Samir Hajji Nuhu, Aggrey Morris, Nadir Haroub Ali 'Canavaro, Sabri Ali, Khamis Mcha 'Vialli', Abdulaghan Gulam, Jaku Juma, Seif Abdallah/Adeyom Saleh Ahmed dk88 na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
Rwanda; Jean Claude Ndoli, Emery Bayisenge, Hamdani Bariyanga, Ismail Nshutiyamagara, Mwemere Ngirishuti/Jean Claude Iranzi dk46, Jean Baptiste Mugiraneza, Haruna Niyonzima, Jimmy Mbagara, Jerome Sina, Jean D’Amour Uwimana/Fabrice Twagizimana dk24 na Tumaine Ntamuhanga/Dadi Birori dk66.


MSIMAMO KUNDI C:
                     P   W  D   L    GF GA GD Pts
Zanzibar        2    1    1    0    2    1    1    4
Rwanda         2    1    0    1    3    2    1    3
Malawi           2    1    0    1    3    4    -1  3
Eritrea           2    0    1    1    2    3    -1  1

Beki wa Zanzibar, Nassor Masoud 'Chollo' akiondoka na mpira mbele ya kiungo wa Rwanda, Haruna Niyonzima

Kikosi cha Rwanda leo

Kikosi cha Uganda leo

Vialli kushoto akishangilia bao lake la pili, kulia ni Suleiman Kassim 'Selembe' 

Wachezaji wa Zanzibar wakishangilia bao la pili kwa staili ya kupiga kasia

No comments:

Post a Comment