Pages

Thursday, January 3, 2013

MAPINDUZI CUP: SIMBA YAIBUTUA GOLI 4 JAMHURI YA PEMBA TUSKER NAYO YATOA KIPIGO




 MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba SC wameanza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuwachapa mabingwa wa Zanzibar, Jamhuri ya Pemba mabao 4-2 usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.  
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana mabao 2-2, zikicheza huku zikinyeshewa na mvua iliyoanza kabla hazijaingia uwanjani.
Jamhuri ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 17, mfungaji Mfanyeje Mussa Yussuf kwa shuti la umbali wa mita 17.
Simba ilisawazisha bao hilo dakika ya 27, mfungaji Haruna Athumani Chanongo aliyeunganisha kwa kichwa kona maridadi iliyochongwa na kiungo Kiggi Makassy kutoka wingi ya kulia.
Baada ya bao hilo, Simba walizidisha mashambulizi langoni mwa Jamhuri na iliwachukua dakika mbili zaidi kupata bao la kuongoza, baada ya Chanongo kufumua shuti kali akiwa umbali wa mita 20 upande wa kushoto mwa Uwanja, ambalo lilimshinda mlinda mlango Jaffar Said.
Huku ikielekea kama Simba itatoka uwanjani baada ya ngwe ya kwanza ikiwa inaongoza 2-1, Mfanyeje tena aliwainua vitini wapenzi wa timu hiyo ya Chasasa, Pemba kwa bao tamu la kusawazisha akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Abdallah Athumani, akamtungua kiulaini kipa wa Simba, William Mweta.    
Kipindi cha pili, Simba walirudi kwa kasi ya kusaka bao la ushindi iliwachukua dakika 12 tu kufanikisha malengo yao, baada ya Nahodha wa timu hiyo leo, Shomary Kapombe aliyecheza kama kiungo mkabaji badala ya beki wa kati, kufunga kwa shuti la chini la mpira wa adhabu.
Adhabu hiyo ilifuatia mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr.  kufanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la hatari na beki mmoja wa Jamhuri.
Sunzu aliwainua vitini wapenzi wa Simba dakika ya 66, baada ya kuuwahi mpira uliokuwa unaelekea kutoka nje na kugeuka nao kuutumbukiza nyavuni kiufundi.
Kabla ya mchezo huo, Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad alizindua mashindano hayo kwa kupiga penalti na kumfunga kipa wa Jamhuri, Jaffar. Akiongozwa na raisi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Aman Ibrahim Makungu, Mh Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alizikagua timu zote mbili kabla ya kuanza kucheza.
Kocha mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig alikuwa jukwaani akiishuhudia timu, ikiongozwa na watakaokuwa wasaidizi wake, Mganda Moses Basena na mzalendo, Jamhuri Kihwelo.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Mussa Mudde/Abdallah Seseme dk81, Komabil Keita, Shomary Kapombe, Haroun Chanongo, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude 67, Felix Sunzu/Ramadhan Singano dk81, Haruna Moshi na  Kiggi Makassy/Christopher Edward dk27.
Jamhuri FC; Jaffar Said/Suleiman Maabad dk 75, Msafiri Leonard, Hamad Omar, Hussein Omar, Mfaume Shaaban, Soud Amoud, Bakari Hamisi, Ally Bilal/Mbara Ali dk82, Ally Ahmed ‘Shiboli’, Mfanyeje Mussa na Abdallah Athumani.
Katika mchezo uliotangulia, Tusker ya Kenya iliichapa Bandari ya hapa mabao 5-1, mabao ya Jesse Were 29 na 43, Ismail Dunga 35 Michael Olunga dakika ya 89 na Andrew Tolowa dakika ya 90, wakati la Bandari lilifungwa na Amour Janja dakika ya 83.

No comments:

Post a Comment