Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba
WATU
wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamevamia nyumbani kwa Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba kwa lengo la kufanya
uhalifu. Hata hivyo majambazi hao ambao walimfunga kamba mlinzi wa
nyumba hiyo na...
kuingia
ndani, hawakufanikiwa kuiba chochote. Naibu Waziri Makamba aliliambia
gazeti hili kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana wakati yeye
akiwa safarini jimboni kwake Bumbuli ila familia yake ilikuwapo nyumbani
hapo.
Makamba alisema baada ya majambazi hao kuingia ndani, walimfunga kamba na kumziba mdomo mlinzi.
“Ujambazi
huo ulitaka kufanyika nyumbani kwangu Masaki karibu na Ubalozi wa
Afrika Kusini. Mimi sikuwepo nyumbani. Walivamia chumbani mke wangu
akabonyeza kengele iliyopiga kelele ndio wakakimbia, baada ya majirani
kuwasili eneo la tukio, wakatokomea kusikojulikana,” alisema Makamba na
kuongeza:
“Waliingia
kwenye ofisi yangu ya pale nyumbani na kupekua. Lakini cha ajabu ni
kwamba sebuleni kulikuwa na Ipad na laptop (kidadavuzi mpakato) lakini
hawakuvichukua.”
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyella alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kwamba watu hao walitaka kufanya ujambazi, lakini
hawakufanikiwa.
Kamanda
Kenyella alisema tukio hilo lilitokea saa 10 alfajiri ya kuamkia jana,
lakini majambazi hao hawakufanikiwa kutimiza azima yao.
“Walimfunga
kamba mlinzi na kufungua dirisha, kisha kuingia ndani. Lakini
hawakufanikiwa kuchukua chochote,” alisema Kamanda Kenyella.
Kamanda
Kenyella alieleza kuwa majambazi hao hawakufanikiwa kuiba chochote kwa
kuwa wakazi wa eneo hilo, walisikia purukushani na kupiga kelele
zilizosababisha watu hao kutokomea.
“Haijulikani
walikuwa wangapi kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewaona, lakini katika
tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa,” alisema Kamanda Kenyella.
Alisema
baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi Kinondoni, inaendesha msako wa
kuwatafuta watu hao ili kuweza kuwatia nguvuni na kuwafikisha
mahakamani.
No comments:
Post a Comment