MBUNGE
wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba (CCM) jana aliibana Serikali na
kuitaka itamke kufuta suala la uzoefu kwa watu wanaoomba ajira mpya.
Nchemba alitoa kauli hiyo katika swali lake kwa Waziri Mkuu ambapo
alisema Tanzania hakuna chuo kinachofundisha masuala ya uzoefu kazini.
Mbunge huyo ambaye ni Naibu Katibu Mkuu (CCM) Bara, alielezwa kukerwa
kwake na kitendo cha utitiri wa viongozi wanaokaimu nafasi zaidi ya
mbili ilhali wapo vijana ambao hawana kazi.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, taasisi za Serikali zimekuwa na utaratibu wa
kuwataka watu wanaoomba ajira wawe na uzoefu wakati kuna upungufu mkubwa
wa watumishi mpaka Tume ya Mipango, wakati huohuo wasiokuwa na kazi ni
wengi ni kwa nini suala la uzoefu linakuwa ni kikwazo?” alihoji Nchemba.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikiri kuwa ni kweli
Tanzania kuna upungufu mkubwa wa watumishi na hasa kada ya ualimu na
afya.
Alisema kuwa Serikali inatumia taratibu mbalimbali kwa ajili ya kumaliza
matatizo ya upungufu wa watumishi ukiwamo kuajiri wapya huku akisema
kuwa upungufu wa walimu utakuwa ni mgumu kuisha mapema kutokana ongezeko
kubwa la wanafunzi kwa sasa.
Wakati huohuo, Serikali inakusudia kupeleka bungeni muswada wa sheria
ili kuifanyia marekebisho sheria iliyotungwa kuhusu Hifadhi na
Ngorongoro.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alisema kuwa
kilio cha wenyeji wa Ngorongoro ni cha msingi na hivyo kinapaswa
kusikilizwa.
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la papo kwa hapo kutoka kwa Mbunge
wa Viti Maalumu Nameok Sokoine ambaye alihoji taratibu zinazochukuliwa
na Serikali katika kulishughulikia tatizo la wananchi wa Ngorongoro
ambao wanakabiliwa kwa kiasi kikubwa na njaa.
Sokoine alisema Serikali haikuwatendea haki wananchi wa Ngorongoro kwa
kubadilisha matumizi ya ardhi yao bila ya kuwashirikisha licha ya kuwa
wameishi katika maeneo hayo hata kabla ya ukoloni.
No comments:
Post a Comment