Na. Emmanuel J. Shilatu
Mara
baada ya kufanikiwa kuziondoa tawala mbovu, nyonyaji na za kidhalimu za
Wakoloni hapa nchini, aliyekuwa akiongeza harakati hizo ambaye pia ni
Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema ya kuwa
“tumefanikiwa kuwaondoa wakoloni na hivyo tupo huru na Uhuru ni kazi”.
Hapa Mwalimu Nyerere alikuwa na maana ya kuwa ili tuweze kupiga hatua
kimaendeleo ni lazima tuutumie huu uhuru wetu vilivyo kwa kufanya kazi
kwa bidii na maarifa yote ili kuleta maboresho katika Nyanja zote za
kimaisha yaani uchumi, kijamii na kisiasa.
Na ndio maana yeye kama kiongozi alianza kuonyesha mfano wa dhahiri
kwa kuanzisha mapambano kwa vitendo dhidi ya maadui zetu watatu ambao
ni ujinga, maradhi, na umaskini. Sehemu ya mafanikio yake ni kwa kupitia
kuanzisha maazimio, mashirika, kauli mbiu na sera mbalimbali. Hayo
yoote (yaani tangu kusaka uhuru wa Tanganyika) aliweza kufanikiwa
kutokana na kufanya mambo kwa matendo zaidi kuliko maongezi (porojo)
zisizoisha.
Pia
Mwalimu Nyerere alikuwa na falsafa (dhana) ya kimaendeleo ambapo
aliamini kuwa maendeleo sahihi hayawezi yakapatikana nje ya uwepo wa
mambo manne ambayo ni“Watu”, “ardhi”, “siasa safi”na “uongozi bora”
Ndio
“Watu”ni kiungo kimojawapo cha hakikisho la maendeleo chanya yeyote
yale ndani ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla. Kama tutakuwa na
miundombinu bora ni watu wamechangia uwepo wake; kama tutakuwa na mazao
ya kutosha kwa ajili ya chakula, kiada na biashara ni watu ndio
wamechangia hayo; Endapo kuna amani na utulivu nchini basi ujue watu
wamechangia hayo; ama taifa likiwa na wasomi wa kutosha ni watu
mbalimbali ndio wamechangia hilo.
Licha
ya kwamba Taifa letu Tanzania lina watu zaidi ya Milioni 45 lakini hao
watu wamekuwa ndio kikwazo kikubwa katika uletaji wa maendeleo ya kweli
na ya dhahiri. Tatizo lililopo ni uibukaji wa umaskini mkubwa wa
utegemezi na utajiri mkubwa wa porojo ndani ya jamii na kila Mwana jamii
ni mwathirika wa hili si Kijana wala Mzee awe ni Mwanamke au Mwanaume.
Utakuta
vijana wengi kutwa wanashinda kwenye kucheza “pool table” na kukaa
vijiweni tu; Wazee ama akina Baba nao kutwa wanacheza “bao” ama “draft”
tu; na akina Mama nao kila kukicha wapo vibarazani wakisutana na
kupashana umbea tu. Hayo ndio maisha ya kila siku ya baadhi ya wanajamii
ya kutokupenda kufanya kazi kwa bidii.
Jamii inachojua ni utegemezi pekee. Kivipi? ... Kwa
jinsi tuanavyoishi utadhani tunawangojea baadhi ya watu kutoka nje ili
waje watuletee maendeleo yaani imefika kipindi kwa mtu hata kutandika
kitanda chake mwenyewe anacholalia imekuwa ni kazi kuubwa kwake. Pia
suala la maendeleo ya nchi yetu wenyewe tumewaachia viongozi pekee huku
tukijiengua katika kapu la dhana ya neno“Serikali” wakati kiuhalisia na
kikatiba pia ni kwamba Serikali inaundwa na viongozi pamoja na Wananchi.
Hii
yote inatokana na jamii kuziasi mitazamo miongozo na falsafa za Mwalimu
Nyerere (mathalani ile ya “Uhuru ni kazi”) hali inayosababisha kiwango
cha idadi ya watu maskini kuzidi kukua nchini licha ya kujaariwa
rasilimali na mali za asili kwa kuyachakachua maendeleo yetu wenyewe.
Kisa? Porojo kutawala maisha yetu.
Hali
hii tuliyonayo ya kutaka kuongea ongea ovyo huku parojo zikituendesha
katika masuala ya kimsingi ya maisha yetu, tunataka tuwaambukize hata na
viongozi wetu. Imefika kipindi kigezo ama kipimo cha uwezo wa Kiongozi
unapimwa na utokeaji wa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari ama
uongeaji, uropokaji na ubwatukaji wa mara kwa mara kwenye jumba letu
tukufu la kutunga sheria na wala si utendaji wake kazi na uletaji wa
maendeleo katika jamii yaani ni usanii, usanii mtupu. Hii ni hatari
sana.
Hivi
tunachotaka kutoka kwa Kiongozi ni mazungumzo pekee ama matendo yake ya
kimaendeleo? Ama uwezo wa kiongozi bora upo kwenye mazungumzo tu ama
utakelezaji wa kimaemdeleo? Hivi uhodari wa mbunge wangu unatoka na
amezungumza mara ngapi Bungeni ama amenipunguziaje zigo langu la
matatizo ya kimsingi? Bila shaka majibu ni hapana ila ajabu ya firauni
ni kuwa kwa miaka ya hivi karibuni kumeibuka dhana mfu ya kupima
uwezo wa Kiongozi si kwa uletaji wa maendeleo bali ugwiji wake wa
kuzungumza Bungeni kwa kuchangia hoja kuulizwa maswali ya msingi na
kadhalika.
Mtazamo
huu unaonyesha kuwa kiongozi bora anapimwa kwa uwezo wake wa kuongea
Bungeni na si utetaji wa maendeleo; Pili, wanawafundisha viongozi wetu
tabia mbaya ya kuwa wawe ni wazungumzaji tu na si watendaji; Tatu,
inavyoonyesha hawaijali thamani ya maisha ya Mtanzania bali ya Yule
anayeiwasha vipaza sauti mara kwa mara pale mjengoni.
Katika
kipindi fulani cha nyuma tafiti mojawapo nchini walitoa matokeo yao ya
utafiti ambapo waliueleza Umma kuwa Mh. Edward Ngoyai Lowassa ndiye
anayeongoza pale Bungeni kwa kutokuongea pale Bungeni tangu 2005. Jamani
hivi ni kweli?
Lowassa
wanayemzungumzia ni yule yule ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza
katika serikali hii ya awamu ya nne kwa takribani miaka miwili.
Kikatiba, Waziri Mkuu ndiye Kiongozi wa shughuli nzima za Serikali
Bungeni. Hivi inawezekana vipi kwa kiongozi mkubwa kama huyo (Waziri
Mkuu) kutokuongea lolote lile kwenye mikutano na vikao vya Bunge? Amu
hoja au maswali mazito yahusuyo serikali yakiwashinda Mawaziri, M/Waziri
au Mwanasheria Mkuu huwa yanatolewa ufafanuzi na nani?
Suala
la kuongea mno Bungeni sio hoja ya kuwaletea neema ya kimaendeleo bali
Wapiga kura wanahitaji matendo na wala sio maneno matupu . Wapo Wabunge
ambao sio waongeaji lakini kwenye majimbo yao wameleta neema ya ajabu
kupitia uongozi wao.
Mathalani
Mh. Nimrod Mkono ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini katika kipindi cha
ubunge wake amewaletea neema kubwa Wapiga kura wake. Amewajengea shule
ya sekondari kubwa na ya kisasa na kuikabidhi kwa Serikali, amejenga
maabara ya kisasa iliyojitosheleza kila kitu mihimu,
amejenga nyumba za walimu. Pia amewanunulia gari la kubebea wagonjwa kwa
wana wa jimbo la Musoma vijijini na kadhalika. Pamoja na kutokuongea
kwake Bungeni lakini Wapiga kura wake hauwaelezi kitu kwani ni Mkono,
Mkono tu. Hivyo kutokuongea Bungeni sio tatizo.
Pia
mwangalie Mohamed Dewji “MO” (Mbunge wa Singida Mjini) ambaye yeye si
muongeaji lakini nyakati zote ameonyesha nia ya dhati ya kuwapenda na
kuwathamini wapiga kura wake. “MO” amejitolea kwalipia ada ya vyuoni
wale wote wa jimbo lake waliobahatika kupata elimu ya juu (chuoni), kwa
wale pia ambao wana vigezo amewaahidi kuwapa ajira za kudumu kupitia
makampuni yake, hata hivyo pia amekamilisha miradi mingi ya maendeleo
ambayo ilikuwa inasuasua.
Hao
ni baadhi tu ya wale ambao sio waongeaji lakini ni watendaji haswaa
ambao Wapiga kura wao wanajivunia nao. Lakini wapo wale ambao ni mafundi
wa kuongea hadi kuwa wabwatukaji pale Bungeni lakini uongeaji wao huo
haujawasaidia lolote lile Wapiga kura wao.
Licha
ya ufundi wao wa kuongea lakini wameshindwa kuwatatulia kero za maji,
umeme, hospitali, shule ama masoko kwa ajili ya bidhaa zao; wengine
waliahidi kuwajengea majosho ya kuogesha ng’ombe wao, kuwajengea
machinjio ya kisasa na hata wengine wameshindwa kuikamilisha mradi wa
ujenzi wa kawaida cha kusindika Tangawizi tu. Wengine ndio wameua kabisa
sekta ya kilimo katika majimbo yao hali ambayo inawafanya Wananchi
waishi maisha magumu na yasiyoelezeka.
Nimelazimika
kuyaeleza haya kutokana na mitazamo isiyo na tija kwa jamii inayozaa
matukio ya uletaji ushabiki wa kisiasa kwenye chombo muhimu cha kutunga
sharia za nchi ambapo Wabunge wanawatelekeza wapiga kura wao kwa
kutokupigania maslahi yao na badala yake wanaendekeza ushabiki wa
kichama ndani ya Bunge.
Ni
aibu isiyoelezeka kumuona Mbunge anawasha kipaza sauti na kuanza kutoa
maneno ya kebehi kwa kufuata utashi wa kisiasa. Huko ni kuwapotezea muda
wapiga kura wao.
Dhana
ya hiyo ya kushabikia waongeaji ndani ya Bunge imewafanya Wabunge wengi
wasiwe watiifu mbele ya kiti cha Spika kwa kujiamulia kuwasha vipasa
sauti na kila mmoja kuanza kuzungumza na hatimaye kuligeuza Bunge kuwa
gulio na si tena mhimili wa dola.
Utoto
wa Wabunge haustahili kuvumiliwa hata kidogo kwa kuwa wao ni Watu
wazima na watu wamewaamini kiasi cha kuwapatia madaraka.
Endapo
Mbunge atakuwa anatumia muda mwingi kwa ajili ya kuzomea zomea ndani ya
Bunge ama kutoa lugha za kebehi na dharau ndani, atapata wapi wasaa wa
kuwasemea matatizo ya Wapiga kura wao? Je, sisi Wananchi wa kawaida
tunanufaikaje na matokeo hayo ya kitoto yanayofanywa na Wabunge wetu
tuliowachagua?
Kimsingi,
umaarufu wa Mbunge hauji kwa kuzunumza kwa jazba wala kutoa lugha za
maudhi awapo Bungeni, umaarufu wa Mbunge utatokana na kutekeleza ahadi
ahadi ya kukidhi matarajio kwa waliomchagua.
Ni
vyema Wabunge wakatambua ya kwamba fursa na uhuru waliopewa na watu
waliowaamini una mipaka na una mwisho wake, ni vyema wakautumia huo
uhuru kabla wakati haujawapita kwani wakati ni ukuta, wakishindana nao
wataumia.
Ndugu
zangu, kuna haja kubwa ya kuwa makini sana wakati wa upigaji kura ili
kuepukana na wabunge wasijali maslahi ya Wananchi bali maslahi yao na ya
chama chao, kuwaepuka viongozi watovu wa nidhamu dhidi ya kanuni na
utaratibu husika. Bila ya hivyo, tutazidi kuwa maskini!
Mwandishi wa makala hii anapatikana kupitia:www.ndgshilatu.blogspot.com
No comments:
Post a Comment