CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuna mpango mchafu wa kuwabambikizia viongozi wakuu wa chama hicho kesi ya kumwagiwa Tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Musa Tesha.
Viongozi wanaoandaliwa mpango huo ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Mnyika alisema mpango huo unafanyika kwa lengo la kukidhoofisha chama chao kinachowapa wakati mgumu CCM.
Alisema hivi sasa baadhi ya makachero wa polisi wamekuwa wakiwakamata vijana na kuwalazimisha kukiri kwa kuandika au kuandikiwa maelezo kuwa viongozi hao waliwatuma kummwagia tindikali Tesha wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
Mnyika alisema wafuasi wao waliokamatwa na polisi kwa kuhusishwa na tukio hilo wameshinikizwa kusema Mbowe, Slaa, Lissu na yeye ndio waliowatuma kummwagia tindikali Tesha.
Alisema jambo hilo linaendeshwa kisiasa, ambapo wafuasi wanne wameshatiwa mbaroni na kuwalazimisha kuwataja viongozi wakuu wa CHADEMA kuhusika na uhalifu huo.
Mnyika aliwataja waliokamatwa ni pamoja na Evodius Justinian, aliyeshikiliwa kwa siku mbili mjini Bukoba, na baadaye akapelekwa Mwanza kabla ya kufikishwa Dar es Salaam.
Alisema zoezi hilo lilifanyika kwa kificho na mtuhumiwa huyo baadae alifikishwa Igunga.
Alibainisha kuwa taarifa za kada huyo kupelekwa Dar es Salaam zilikuwa za kificho kwani wakili wake, Nyaronyo Kicheere aliyeongozana na ndugu wa mtuhumiwa huyo walipofika Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam walielezwa amepelekwa Makao Makuu.
Mnyika alisema mara baada ya Evodius kuonana na wakili wake, Kicheere, siku hiyo alieleza unyama aliofanyiwa na jeshi hilo wakati wote wa mahojiano mkoani Mwanza na Dar es Salaam.
Katika maelezo yake yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Advocate Nyombi, Evodius alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa siri bila ndugu zake kujua, alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila kuruhusiwa kuonana na wakili wake.
Kada huyo akisimulia unyama aliofanyiwa alisema: “Nimepigwa na polisi Mwanza, nikiwa chooni Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati naletwa huku, polisi wakaniambia mimi ni mtu hatari sana, niseme nilifanya nini Igunga na kama najua mkanda wa Lwakatare.
“Nikiwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni, waliingia pamoja na mimi wakanipiga sana, nimeshaandika maelezo kwa kulazimishwa, niliomba kuwa na wakili wakanikatalia.”
Aliongeza kuwa akiwa Dar es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video ya Lwakatare. Akawajibu kuwa ilifanyiwa uhariri na Ludovick, lakini akapigwa makofi na askari wakaagiza nyaya za umeme za kutesea.
“Waliposimama kuleta nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme nikasema hii video ni yangu. Ninaumwa sana tumbo la kuhara damu, natumia dawa nilizonunuliwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kagera tarehe 4 Aprili,” alisema.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa pili aliyeteswa ili akubali kuandika kuwa Mbowe, Slaa, Lissu na Mnyika walimtuma akammwagie tindikali Tesha ni Seif Kabuta aliyekamatwa Mwanza.
Alisema Kabuta baada ya kukataa kukiri kuwa viongozi wake wanahusika na matendo hayo, walimfungia katika chumba maalumu wakamleta mke wake, mama yake na mkwe wake na kumtesa mbele yao ili akiri kuwa Mbowe na wenzake walimtuma kummwagia Tesha tindikali.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa tatu aliyekamatwa kuhusishwa na tindikali ni Oscar Kaijage wa Shinyanga mjini, ambaye awali alipokamatwa aliambiwa ni kwa sababu kuna pesa zimepotea kwa njia ya simu, na yeye alikuwa anajishughulisha na uwakala wa pesa kwa njia ya mitandao ya M-pesa na Z-pesa.
Alisema mtuhumiwa huyo alipokutanishwa na makachero wa polisi makao makuu, naye alilazimishwa aseme kuwa Mbowe, Slaa, Lissu na Mnyika walimtuma akammwagie Tesha tindikali.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa nne ni Rajab Kihawa, aliyetumiwa wasichana kuitwa akiwa Dodoma, ambaye aliombwa akubali kupewa shilingi milioni 30, kama alivyolipwa Ludovick ili aseme kuwa Mbowe na wenzake waliwatuma kummwagia tindikali Tesha.
Mtuhumiwa wa mwisho ni Henry Kilewo, Katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya Kinondoni, na Katibu wa Makatibu wa CHADEMA Kanda Maalumu ya Dar es Salaam anayeshikiliwa na polisi.
Polisi wanamtuhumu Kilewo kummwagia tindikali Tesha wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
Kilewo alishikiliwa na polisi kuanzia Ijumaa iliyopita na baada ya kuhojiwa alichukuliwa kwa kificho kupelekwa Mwanza kwa ndege ili aweze kuunganishwa katika kesi hiyo ya Igunga leo.
Mnyika alisema Kilewo amesafirishwa bila wakili wake kuwa na taarifa kuwa amepelekwa Mwanza, wala mke wake aliyeambiwa ampelekee chakula, lakini alipofika polisi aliambiwa mume wake hayupo.
Mmoja wa mawakili wanaokwenda Igunga kuwatetea Kilewo na wenzake, Profesa Abdallah Safari alisema wameshitushwa kusikia wateja wao wamelazimishwa kutoa maelezo ili kuwahusisha viongozi wakuu wa CHADEMA.
Alibainisha kuwa kutokana na kesi hiyo kuonekana kujaa masuala ya kisiasa, atashirikiana na mawakili wenzake ambao ni Peter Kibatala na Gasper Mwalyela na kama itakapolazimika watawaongeza Mabere Marando, Kicheere, Method Kimomogoro na Lissu.
Aliongeza kuwa imefika hatua itabidi atumie kifungu cha sheria cha 102, ili kujenga dhana ya kutiliwa shaka kwani viongozi wote wa CHADEMA sasa wamefunguliwa kesi katika maeneo mbalimbali nchini, huku wale wa CCM wakiachwa.
Profesa Safari alitolea mfano Mbunge wa Tabora mjini, Ismail Aden Rage, ambaye alipatwa na hatia katika uchaguzi wa Igunga na alipaswa kufungwa miaka mitatu bila fidia, lakini DPP amekalia faili lake hadi sasa.
Aliongeza kuwa mambo hayo yanajitokeza kutokana na CHADEMA kumtaja ofisa wa usalama anayeitwa Shaali Ally kuwa ndiye aliwatafuta vijana wa chama hicho akiwemo Ahmed Sabula na wenzake.
Alibainisha kuwa Machi 29, mwaka huu vijana hao waliitwa na Shaali katika chumba cha hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam, akiwataka wakubali kutumika kwa kutoa taarifa za vikao vya CHADEMA, kuwasilisha kwake nyaraka za kamati kuu na kueleza mipango ya chama katika kesi ya Lwakatare.
Kwenye mpango huu, ofisa huyo wa usalama wa taifa ambaye Marando alisema anamfahamu vizuri, alimuahidi Sabula kiasi cha sh milioni 30 na kwamba fedha hizo angelipwa kama ujira kwa kukubali kutoa ushahidi dhidi ya Lwakatare.
Tanzania Daima
HALMASHAURI YA JIJI LA DAR ES SALAAM YAKIMBIZA WAHUNI WOTE KWENYE MIRADI YA
SERIKALI
-
Halmashauri ya jiji la Dar es salaam imefuta mikataba yote ya ujenzi ambayo
imekuwa ikisuasua katika utekelezaji na kuisababishia halmashauri hasara
kubw...
3 hours ago
No comments:
Post a Comment