CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuna mpango mchafu
wa kuwabambikizia viongozi wakuu wa chama hicho kesi ya kumwagiwa
Tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Musa Tesha.
Viongozi wanaoandaliwa mpango huo ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu
Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Mnyika alisema mpango huo unafanyika
kwa lengo la kukidhoofisha chama chao kinachowapa wakati mgumu CCM.
Alisema hivi sasa baadhi ya makachero wa polisi wamekuwa wakiwakamata
vijana na kuwalazimisha kukiri kwa kuandika au kuandikiwa maelezo kuwa
viongozi hao waliwatuma kummwagia tindikali Tesha wakati wa uchaguzi
mdogo wa Igunga mwaka 2011.
Mnyika alisema wafuasi wao waliokamatwa na polisi kwa kuhusishwa na
tukio hilo wameshinikizwa kusema Mbowe, Slaa, Lissu na yeye ndio
waliowatuma kummwagia tindikali Tesha.
Alisema jambo hilo linaendeshwa kisiasa, ambapo wafuasi wanne
wameshatiwa mbaroni na kuwalazimisha kuwataja viongozi wakuu wa CHADEMA
kuhusika na uhalifu huo.
Mnyika aliwataja waliokamatwa ni pamoja na Evodius Justinian,
aliyeshikiliwa kwa siku mbili mjini Bukoba, na baadaye akapelekwa Mwanza
kabla ya kufikishwa Dar es Salaam.
Alisema zoezi hilo lilifanyika kwa kificho na mtuhumiwa huyo baadae alifikishwa Igunga.
Alibainisha kuwa taarifa za kada huyo kupelekwa Dar es Salaam zilikuwa
za kificho kwani wakili wake, Nyaronyo Kicheere aliyeongozana na ndugu
wa mtuhumiwa huyo walipofika Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
walielezwa amepelekwa Makao Makuu.
Mnyika alisema mara baada ya Evodius kuonana na wakili wake, Kicheere,
siku hiyo alieleza unyama aliofanyiwa na jeshi hilo wakati wote wa
mahojiano mkoani Mwanza na Dar es Salaam.
Katika maelezo yake yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu,
Advocate Nyombi, Evodius alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa
siri bila ndugu zake kujua, alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila
kuruhusiwa kuonana na wakili wake.
Kada huyo akisimulia unyama aliofanyiwa alisema: “Nimepigwa na polisi
Mwanza, nikiwa chooni Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati naletwa
huku, polisi wakaniambia mimi ni mtu hatari sana, niseme nilifanya nini
Igunga na kama najua mkanda wa Lwakatare.
“Nikiwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni,
waliingia pamoja na mimi wakanipiga sana, nimeshaandika maelezo kwa
kulazimishwa, niliomba kuwa na wakili wakanikatalia.”
Aliongeza kuwa akiwa Dar es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video
ya Lwakatare. Akawajibu kuwa ilifanyiwa uhariri na Ludovick, lakini
akapigwa makofi na askari wakaagiza nyaya za umeme za kutesea.
“Waliposimama kuleta nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme
nikasema hii video ni yangu. Ninaumwa sana tumbo la kuhara damu, natumia
dawa nilizonunuliwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa
Kagera tarehe 4 Aprili,” alisema.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa pili aliyeteswa ili akubali kuandika kuwa
Mbowe, Slaa, Lissu na Mnyika walimtuma akammwagie tindikali Tesha ni
Seif Kabuta aliyekamatwa Mwanza.
Alisema Kabuta baada ya kukataa kukiri kuwa viongozi wake wanahusika na
matendo hayo, walimfungia katika chumba maalumu wakamleta mke wake, mama
yake na mkwe wake na kumtesa mbele yao ili akiri kuwa Mbowe na wenzake
walimtuma kummwagia Tesha tindikali.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa tatu aliyekamatwa kuhusishwa na tindikali ni
Oscar Kaijage wa Shinyanga mjini, ambaye awali alipokamatwa aliambiwa
ni kwa sababu kuna pesa zimepotea kwa njia ya simu, na yeye alikuwa
anajishughulisha na uwakala wa pesa kwa njia ya mitandao ya M-pesa na
Z-pesa.
Alisema mtuhumiwa huyo alipokutanishwa na makachero wa polisi makao
makuu, naye alilazimishwa aseme kuwa Mbowe, Slaa, Lissu na Mnyika
walimtuma akammwagie Tesha tindikali.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa nne ni Rajab Kihawa, aliyetumiwa wasichana
kuitwa akiwa Dodoma, ambaye aliombwa akubali kupewa shilingi milioni 30,
kama alivyolipwa Ludovick ili aseme kuwa Mbowe na wenzake waliwatuma
kummwagia tindikali Tesha.
Mtuhumiwa wa mwisho ni Henry Kilewo, Katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya
Kinondoni, na Katibu wa Makatibu wa CHADEMA Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam anayeshikiliwa na polisi.
Polisi wanamtuhumu Kilewo kummwagia tindikali Tesha wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
Kilewo alishikiliwa na polisi kuanzia Ijumaa iliyopita na baada ya
kuhojiwa alichukuliwa kwa kificho kupelekwa Mwanza kwa ndege ili aweze
kuunganishwa katika kesi hiyo ya Igunga leo.
Mnyika alisema Kilewo amesafirishwa bila wakili wake kuwa na taarifa
kuwa amepelekwa Mwanza, wala mke wake aliyeambiwa ampelekee chakula,
lakini alipofika polisi aliambiwa mume wake hayupo.
Mmoja wa mawakili wanaokwenda Igunga kuwatetea Kilewo na wenzake,
Profesa Abdallah Safari alisema wameshitushwa kusikia wateja wao
wamelazimishwa kutoa maelezo ili kuwahusisha viongozi wakuu wa CHADEMA.
Alibainisha kuwa kutokana na kesi hiyo kuonekana kujaa masuala ya
kisiasa, atashirikiana na mawakili wenzake ambao ni Peter Kibatala na
Gasper Mwalyela na kama itakapolazimika watawaongeza Mabere Marando,
Kicheere, Method Kimomogoro na Lissu.
Aliongeza kuwa imefika hatua itabidi atumie kifungu cha sheria cha 102,
ili kujenga dhana ya kutiliwa shaka kwani viongozi wote wa CHADEMA sasa
wamefunguliwa kesi katika maeneo mbalimbali nchini, huku wale wa CCM
wakiachwa.
Profesa Safari alitolea mfano Mbunge wa Tabora mjini, Ismail Aden Rage,
ambaye alipatwa na hatia katika uchaguzi wa Igunga na alipaswa kufungwa
miaka mitatu bila fidia, lakini DPP amekalia faili lake hadi sasa.
Aliongeza kuwa mambo hayo yanajitokeza kutokana na CHADEMA kumtaja ofisa
wa usalama anayeitwa Shaali Ally kuwa ndiye aliwatafuta vijana wa chama
hicho akiwemo Ahmed Sabula na wenzake.
Alibainisha kuwa Machi 29, mwaka huu vijana hao waliitwa na Shaali
katika chumba cha hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam, akiwataka
wakubali kutumika kwa kutoa taarifa za vikao vya CHADEMA, kuwasilisha
kwake nyaraka za kamati kuu na kueleza mipango ya chama katika kesi ya
Lwakatare.
Kwenye mpango huu, ofisa huyo wa usalama wa taifa ambaye Marando alisema
anamfahamu vizuri, alimuahidi Sabula kiasi cha sh milioni 30 na kwamba
fedha hizo angelipwa kama ujira kwa kukubali kutoa ushahidi dhidi ya
Lwakatare.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment