IKULU ya Marekani na Idara ya Habari (Maelezo),
wametangaza ratiba ya Rais Barrack Obama atakapozuru Tanzania huku
ikionyesha kuwa atakaa siku mbili tu, kuanzia Julai Mosi na kuondoka
kesho yake.
Tanzania itakuwa nchi ya mwisho ya Afrika kutembelewa na Obama baada
ya Senegal na Afrika Kusini. Mara atakapowasili na ndege yake kubwa ya
Air Force One, Rais Obama atazindua barabara mpya katika upande wa
Mashariki wa geti la kuingia Ikulu.
Rais
Obama, ambaye atafuatana mkewe Michelle pia siku hiyohiyo
atazungumza kwa nyakati tofauti na wafanyabiashara kutoka nchi za
Afrika na Marekani kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam. “Pia
amepanga kuzungumza na maofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania,”
ilisema taarifa ya Maelezo.
Baada ya shughuli hiyo, Rais Obama atahudhuria dhifa ya taifa
atakayoandaliwa Ikulu na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete. Siku
itakayofuata ataweka shada la maua kwenye sehemu ulipokuwa Ubalozi wa
Marekani ikiwa ni kumbukumbu ya watu waliofariki katika shambulizi la
bomu mwaka 1998. Pia atatembelea mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya
Symbion na atatoa hotuba akizungumzia mikakati ya Marekani ya kulisaidia
Bara la Afrika kuzalisha nishati ya umeme.
“Tanzania ni mshirika muhimu wa Marekani,” alisema Ofisa wa Ikulu ya
Marekani, Ben Rhodes wakati alipozungumza na waandishi wa habari
mwishoni mwa wiki katika Ikulu ya Marekani kuhusu ratiba ya ziara ya
Obama barani Afrika.
Pia mke wa Obama atakuwa na ratiba yake. Julai Mosi, atapata staftahi
na mwenyeji wake, Salma Kikwete katika ofisi za Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (Wama), Dar es Salaam.
Pia atatembelea sehemu ubalozi wa zamani wa Marekani na baadaye
atashuhudia onyesho la utamaduni la Kikundi cha Baba wa Watoto, ambacho
kinajumuisha watoto wa mitaani wenye umri kuanzia miaka mitano hadi 18
kwenye Makumbusho ya Taifa. Julai 2, atahudhuria mkutano na wake wa
marais wa nchi za Afrika ambao pia utahudhuriwa na mke wa Rais wa zamani
wa Marekani, George Bush, Laura.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment