CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinakabiliwa na hali ngumu sasa
kutokana na laana ya kushindwa kufuata misingi iliyoasisiwa na viongozi
wa chama hicho. Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alitoa kauli hiyo mjini
hapa jana kwenye mkutano mkuu wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima
Tanzania (MVIWATA) unaoendelea. Alisema
waanzilishi wa chama hicho waliwaunganisha wakulima na wafanyakazi na
kufanikiwa kupata uhuru, lakini viongozi wa sasa wamewaweka pembeni watu
hao. “TANU
wakati ule ilifanikiwa kuondoa dola ya mkoloni kwa kuwaunganisha
wakulima na wafanyakazi ingawa haikuwa na polisi wala fedha,” alisema.
Alisema
kwa sasa vyama vinatumia polisi kujiimarisha na hata kutumia fedha
kupata madaraka, hivyo laana hiyo itaendelea kuwatafuna.
“Msijione
wanyonge, ninyi ni mashujaa wa uhuru na wala msikate tamaa…ninyi ni
maaskari wa akiba,” alisema mhadhiri huyo akiwaambia wakulima. Alisema
tatizo lililopo ni kutokana na dola ‘kushirikiana kitanda kimoja’ na
watu wenye fedha, jambo ambalo linasababisha wakulima kuendelea
kudidimia siku hadi siku. Aidha,
alisema Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere alikiri kukosea mambo
mawili ambayo ni kuua vyama vya wakulima pamoja na kutoimarisha uongozi
wa serikali za vijiji na mitaa ambavyo vingekuwa mstari wa mbele
kupigania haki za wakulima nchini. Aliwataka wakulima kupigania vita ya hoja kwa kuwa haiwezekani kuwa na mifumo zaidi ya mmoja katika sekta moja.
No comments:
Post a Comment