Pages

Thursday, July 25, 2013

CCM imelaaniwa - Mhadhiri

  
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinakabiliwa na hali ngumu sasa kutokana na laana ya kushindwa kufuata misingi iliyoasisiwa na viongozi wa chama hicho. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alitoa kauli hiyo mjini hapa jana kwenye mkutano mkuu wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) unaoendelea. Alisema waanzilishi wa chama hicho waliwaunganisha wakulima na wafanyakazi na kufanikiwa kupata uhuru, lakini viongozi wa sasa wamewaweka pembeni watu hao. “TANU wakati ule ilifanikiwa kuondoa dola ya mkoloni kwa kuwaunganisha wakulima na wafanyakazi ingawa haikuwa na polisi wala fedha,” alisema.
Alisema kwa sasa vyama vinatumia polisi kujiimarisha na hata kutumia fedha kupata madaraka, hivyo laana hiyo itaendelea kuwatafuna.

“Msijione wanyonge, ninyi ni mashujaa wa uhuru na wala msikate tamaa…ninyi ni maaskari wa akiba,” alisema mhadhiri huyo akiwaambia wakulima. Alisema tatizo lililopo ni kutokana na dola ‘kushirikiana kitanda kimoja’ na watu wenye fedha, jambo ambalo linasababisha wakulima kuendelea kudidimia siku hadi siku. Aidha, alisema Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere alikiri kukosea mambo mawili ambayo ni kuua vyama vya wakulima pamoja na kutoimarisha uongozi wa serikali za vijiji na mitaa ambavyo vingekuwa mstari wa mbele kupigania haki za wakulima nchini. Aliwataka wakulima kupigania vita ya hoja kwa kuwa haiwezekani kuwa na mifumo zaidi ya mmoja katika sekta moja.

Source:  Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment